Rais wa Venezuela abadilisha tarehe ya Krismasi, maaskofu wampinga

Caracas. Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni. Msemo huu unadhihirishwa nchini Venezuela baada ya Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro kutangaza sikukuu ya Krismasi isherehekewe Oktoba 1.

Kwa kawaida sikukuu ya Krismasi ambayo ni kumbukizi ya kuzaliwa kwa Kristo husherehekewa duniani kote ifikapo Desemba 25 kila mwaka lakini kwa mwaka huu mambo ni tofauti kwa raia wa nchi hiyo huku Rais akidai ni njia ya kuleta amani na furaha kwa taifa.

Maduro (61) amesema sherehe hizo zitaleta amani, furaha na usalama kwa wote, ingawa wachambuzi wa siasa wanasema ni mkakati wa kisiasa wa kudhibiti upinzani katika kipindi hiki ambacho hali ya kisiasa nchini imezidi kuwa mbaya.

“Ni Septemba na tayari inanukia kama Krismasi. Ndio maana mwaka huu, kwa heshima na kwa shukrani kwenu, nitaamuru Krismasi isogezwe hadi Oktoba 1,” amesema Maduro.

Tangazo hilo linakuja wakati kukishuhudiwa mgogoro wa kisiasa baada ya uchaguzi uliofanyika Julai 2024 ambapo Maduro alithibitishwa na Mahakama ya Juu, kuwa mshindi kwa asilimia 52 ya kura kwa mujibu wa Baraza la Taifa la Uchaguzi (CNE).

Ingawa upinzani ukiongozwa na Edmundo Gonzalez, unadai kushinda uchaguzi huo kwa asilimia zaidi ya 60 ya kura. Baada ya Maduro kutangazwa, maandamano yalishuhudiwa huku yakisababisha vifo vya watu 27 na 192 kujeruhiwa huku watu 2,400 wakikamatwa, kulingana na RFI.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya jumuiya ya kimataifa, inayoongozwa na Marekani haitambui kuchaguliwa tena kwa Maduro na upinzani ukisema hautoacha maandamano.

Mmoja ya wakazi wa nchi hiyo, José Ernesto Ruiz, alipohojiwa na Daily Mail amesema si kila mtu anatamani kusherehekea na kuimba nyimbo za Krismasi kwa sasa kutokana na hali ya kifedha na kisiasa inayowakumba wananchi.

Ingawa sio mara ya kwanza kwa Maduro kubadilisha tarehe ya Krismasi tangu kuchukua madaraka ya nchi hiyo yenye Wakatoliki wengi kutoka kwa Hugo Chavez mwaka 2013, alifanya hivyo wakati wa janga la Uvico-19.

Kutokana na hatua ya Maduro, Baraza la Maaskofu wa Venezuela limekosoa tangazo hilo huku likisema sikukuu hiyo haipaswi kutumika kwa malengo ya kisiasa au propaganda. Baraza hilo limesema Krismasi ni Desemba 25, CNN imeripoti.

Related Posts