Aliyefungwa kwa kumbaka bibi kizee miaka 75 aachiwa huru

Mbeya. Mahakama ya Rufani imemwachia huru mkazi wa Kijiji cha Lesyelo, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Lwitiko Mwamkamba, aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka bibi kizee mwenye umri wa miaka 75.

Hii ni baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya chini ya Jaji Joachim Tiganga iliyosikiliza rufaa yake kukubaliana na sababu za rufaa hasa sababu kuu kuwa upande wa mashitaka ulikuwa umeshindwa kuthibitisha shitaka hilo.

Katika hukumu yake aliyoitoa Agosti 30, 2024 na kupakuliwa katika mtandao wa mahakama jioni ya Septemba 4, 2024, Jaji Tiganga aliamuru mshitakiwa aachiliwe mara moja kutoka gerezani, isipokuwa tu kama anashikiliwa kwa makosa mengine.

Bibi huyo katika ushahidi wake, alieleza yeye ana shamba katika Kijiji cha Lyeselo ambako kuna nyumba ambayo huitumia kulala anapokwenda kwa shughuli za shamba na ndipo akadai kubakwa na mrufani Machi 22, 2021.

Alieleza siku hiyo usiku, alikuwa amelala na ndipo alipomsikia mrufani akimwita na kumtaka afungue mlango ili aweze kuifikia njia inayokwenda kwa Magulu (shahidi wa kwanza), lakini alikataa kumfungulia mlango huo.

Baada ya kuona ombi lake limekataliwa, bibi huyo alidai mrufani alisukuma mlango na kuingia ndani na kwa msaada wa mwanga wa taa ya sola, alifanikiwa kumtambua mrufani kwa kuwa wawili hao walikuwa wanafahamiana vilivyo.

Mambo hayakwenda vizuri kwa mujibu wa bibi huyo, kwani mrufani alimwangusha chini na kumkaba shingo, kumvua nguo na kuingiza uume wake katika sehemu zake za siri na wakati anaendelea, ndio akasikia sauti za wapitanjia.

Sauti hizo kwa mujibu wa bibi huyo, ndio zilimfanya amachie na mrufani kukimbia ambapo alifanikiwa kwenda kwa jirani yake ambaye alimpeleka kwa mtoto wake wa kiume na kueleza kila kitu kilichomtokea ndipo baadae mrufani alikamatwa.

Mrufani alivyojitetea kortini

Katika utetezi wake mahakamani, Mwamkamba alikanusha tuhuma hizo na kueleza hakuwahi kumbaka bibi huyo na kueleza alikuwa na mgogoro na mtu aliyemtaja kuwa ni Nuhu katika kilabu cha pombe lakini wakayasuluhisha.

Bila kueleza tukio hilo la ugomvi lilitokea lini, alisema hata hivyo alitokea mtu mwingine na kudai yeye (mrufani) ndiye aliyembaka mama yake.

Hapo alikamatwa na kupigwa sana na kuteswa kabla ya kupelekwa kituo cha Polisi ambapo alilaimika kukiri kumbaka bibi kizee huyo kutokana na hofu ya kuuawa na kuomba haki itendeke na kusisitiza hakuwahi kumbaka bibi huyo.

Badala yake, akaeleza bibi huyo alikuwa amejikanganya mwenyewe kwa kueleza alibakwa Februari 22, 2021 kama hati ya mashitaka ilivyodai tukio lilikuwa Machi 22, 2021 na pia hakuna mtu yeyote aliyeshuhudia akimbaka.

Pamoja na utetezi wake huo, mahakama iliona upande wa mashitaka ulikuwa umeweza kuthibitisha shitaka hilo na kumtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela, ambapo hakuridhika na hukumu hiyo na kuamua kukata rufaa.

Katika kukata rufaa, mrufani huyo aliegemea sababu sita na moja ni kuwa mahakama ilikosema kisheria kumtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 30 bila kutatua suala la namna bibi huyo alivyoweza kumtambua usiku huo.

Hoja nyingine ni kuwa mahakama hiyo ilikosea kumtia hatiani na kumfunga pasipo kuwepo ushahidi wa Jirani wa bibi huyo, na pia bila kupima kama maelezo yake ya onyo ya kukiri kosa aliyatoa polisi, kama aliyatoa kwa mujibu wa sheria.

Halikadhalika alidai kuwa mahakama ilikosea kuzingatia ushahidi wa daktari wa namna alivyomchunguza bibi huyo pasipo kueleza alitumia vifaa gani kumchunguza kama amebakwa na pia Jamhuri ilishindwa kuthibitisha kesi hiyo.

Hata hivyo wakati wa usikilizaji wa rufaa Jamhuri iliwakilishwa na wakili wa Serikali Zena James ambaye alipinga rufaa hiyo akisisitiza kuwa utambuzi wamrufani siku ya tukio ulikuwa wa uhakika (water tight) na alitambuliwa kikamilifu.

Kuhusu kutoitwa kwa Jirani aliyekuwa mtu wa kwanza kumpa msaada, wakili huyo alisema ni msimamo wa sheria kuwa hakuna sharti la idadi fulani ya mashahidi ni lazima waitwe kutoa ushahidi hivyo waliotoa, waliweza kuthibitisha kesi hiyo.

Wakili Zena alisema hata hoja ya maelezo yake ya onyo aliyoyaandika polisi haina mashiko kwa kuwa ilipokelewa mahakamani bila kipingamizi hivyo hoja ya kupokelewa kwa maelezo hayo haiwezi kujitokeza katika hatua ya rufaa.

Kuhusu vifaa vilivyotumika kumpima bibi huyo, wakili huyo alisema msingi wa ushahidi ulikuwa ni kuthibitisha uwepo wa tendo la ngono na hati ya PF3 ilipokelewa pasipo pingamizi na kusisitiza Jamhuri ilithibitisha mashitaka hayo.

Jaji Tiganga alitaja moja ya sababu hiyo ni kutokuwepo kwa maelezo ya kwanini mtuhumiwa kuchelewa kukamatwa na vyombo vya Dola tangu alipotajwa na bibi kizee huyo kuwa ndiye aliyembaka Machi 22, 2021 na kukamatwa Aprili 3, 2021.

Kwa mujibu wa Jaji Tiganga alisema katika kesi hiyo, bibi huyo alimtaja mrufani usiku huo huo na shahidi wa pili akaeleza kuwa alianza kumtafuta hadi alipomkamata, lakini katika ushahidi wake, hakukumbuka alimkamata lini.

“Ukisoma ushahidi wa shahidi wa 4 ambaye ni ofisa wa polisi, mrufani alipelekwa kwake Aprili 3, 2021 ili kuandika maelezo ya onyo. Hii maana yake ndio siku mrufani alidaiwa kukamatwa akituhumiwa kutenda kosa Machi 22, 2021,” alisema.

“Sasa swali ni kuwa kama mrufani alikuwa anafahamiana na shahidi wa kwanza (bibi kizee) na shahidi wa pili, nini ilikuwa sababu ya kuchelewa kukamatwa? Shahidi wa 2 alisema alikuwa anajificha, kwanini aliamini anajificha?” alihoji.

“Pia shahidi wa 2 alisema alikuwa akimtafuta hadi alipomkamata na kumpeleka polisi. Hata hivyo, shahidi huyo hakueleza alikuwa akimtafuta wapi hasa ikizingatiwa alikuwa anafanya kazi Jirani tu na shamba la bibi,” alieleza Jaji.

“Ninaona muda mrefu uliotumika kumkamata mrufani unaibua mashaka kuhusu kutambuliwa na kutajwa kwake mwanzoni. Sheria inasema kutokuwepo maelezo ya kuchelewa kukamatwa kwa mtuhumiwa anayejulikana kunaleta mashaka.”

Jaji alisema hoja nyingine ya rufaa iliyowasilishwa na mrufani ni kutoitwa kwa Jirani ya bibi huyo ambaye ndiye anatajwa alimchukua na kumpeleka kwa shahidi wa 2 usiku huo, lakini Jamhuri ikasema kutoitwa hakukuna na athari kwa kesi.

“Ingawa nakubaliana na wakili wa Serikali juu ya msimamo wa sheria kuhusu kutofungwa juu ya idadi ya mashahidi wanaotakiwa kuthibitisha kosa, lakini naona Jirani huyo alikuwa shahidi muhimu sana wa upande wa mashitaka,” alisema.

“Kwa kuwa ndiye angeweza kusaidia kuondoa mashaka na hasa kwa kuwa mwathirika (bibi) alikwenda kwake usiku ule na kulalamika juu ya kubakwa na mrufani na kumtaja mrufani kuwa ndiye aliyembaka,” alieleza Jaji Tiganga.

Jaji Tiganga alisema kuna ushahidi wa kumpeleka bibi huyo polisi na kupewa PF3 (Fomu ya polisi), lakini si bibi wala shahidi wa pili aliyetoa ushahidi mahakamani kueleza kama waliripoti tukio hilo la ubakaji polisi na walichukua hatua gani.

“Kama polisi walipokea kweli taarifa ya tukio hilo kutoka kwa bibi na shahidi wa pili, kwanini kazi ya kumtafuta mshukiwa wa tukio hilo iliachwa mikononi mwa shahidi wa pili badala ya polisi kufanya wajibu huo?” alihoji Jaji Tiganga.

Jaji akazungumzia kielelezo namba PE1 na PE2 akisema kwa mfano kielelezo PE1 ambapo ni PF3, polisi aliyefungua jalada aliandika kosa ni “anadaiwa kukabawa naomba achunguzwe tupate majibu,” hivyo polisi kosa halikuwa ni kubakwa.

“Kielelezo PE2 ambayo ni maelezo yake, mrufani alidaiwa kueleza alikuwa amemtishia (bibi) kwa kisu wakati anamshambulia. Pia akaeleza kuwa alimkaba mdomo ili asiweze kupiga kelele na alimbaka bibi huyo hadi alipomaliza haja zake,” amesema.

“Lakini shahidi wa kwanza mwenyewe (bibi) hakueleza kabisa hayo mahakamani. Badala yake alieleza kuwa wakati mrufani anaendelea kumshambulia, alisikia wapiti njia wakiongea huko nje na kusababisha mrufani kukimbia,”aliongeza Jaji.

Jaji akahitimisha kwa kusema hitilafu hizo na makosa hayo yanadhoofisha kwa kiasi kikubwa kesi ya mashtaka na kwamba kama mahakama ya chini ingezingatia hayo, isingehitimisha kwa kusema Jamhuri ilithibitisha kosa bila kuacha mashaka.

Kulingana na hitimisho hilo, Jaji akakubaliana na sababu za rufaa za mrufani kuwa mahakama ilikosea kisheria kwa kushindwa kuchambua kwa kina ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri hivyo amebatilisha hukumu na kufuta adhabu aliyopewa.

Related Posts