AKILI ZA KIJIWENI: Tusiikatie tamaa Taifa Stars Afcon

MWANZO haujawa mzuri kwa timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars katika mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 ambazo zitafanyika huko Morocco, mwakani.

Mchezo wake wa kwanza wa kuwania kufuzu fainali hizo katika kundi H dhidi ya Ethiopia ambao tulikuwa nyumbani, Jumatano iliyopita ulimalizika kwa sare tasa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Hayakuwa matokeo mazuri kiuhalisia kwa sababu ushindi wa nyumbani katika mechi kama hizi za makundi ni muhimu kwani mazingira ya Afrika huwa magumu kwa timu kushinda ugenini.

Hata hivyo, licha ya ukweli kwamba matokeo ya sare ya juzi sio ambayo tuliyategemea, hatutakiwi kuanza kukata tamaa mapema hivi na kuiacha timu yenyewe kisa tu haijapata ushindi katika mechi ya kwanza kwenye kundi lake ambalo pia lina Guinea na DR Congo.

Bado kuna mechi tano mbele yetu za kujiuliza baada ya sare ile ya juzi ambazo kama tukijipanga vizuri, tiketi ya kushiriki Afcon 2025 itakuwa mkononi mwetu kwa vile tutavuna pointi ambazo zitatuhakikishia kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye kundi letu.

Kuanza kwa sare au hata kama tungepoteza haitoi uhalali wa kuanza kujipa imani haba kwamba tumeshapoteza tiketi ya kushiriki Afcon mwakani kwa vile mechi tano zinaweza kubadilisha taswira ya kundi ama kwa Stars kuongoza au kumaliza katika nafasi ya pili.

Mchezo wa juzi dhidi ya Ethiopia unapaswa kutuamsha usingizini na kutukumbusha kuwa kwa sasa soka duniani limebadilika na hakuna timu rahisi tena hivyo tunavyokuwa na malengo ya kucheza Afcon tunapaswa kuheshimu kila mpinzani ambaye tutakutana naye.

Mazoea hujenga tabia hivyo kama tutaweka utaratibu wa kuheshimu timu pinzani na kuziandaa vyema timu zetu pindi zinaposhiriki mashindano tofauti hapana shaka tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Mwisho kabisa hatutakiwi kukubali unyonge baada tu ya matokeo ya mchezo wa kwanza. Tuamini nafasi ya kurekebisha ipo na mechi zijazo tutang’ara.

Related Posts