Anayetajwa ‘afande’ atinga mahakamani, kesi yaahirishwa

Dodoma. Fatma Kigondo anayelalamikiwa kuwatuma watuhumiwa wa kosa la kubaka kwa kundi ametii wito wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma iliyomtaka kufika mahakamani hapo leo Septemba 5, 2024. 

Mahakama hiyo Agosti 23 ilitoa wito wa kufika mahakamani (samansi) kwa Fatma baada ya ile ya awali iliyomtaka kuhudhuria mahakamani siku hiyo kutotekelezwa.

Shauri hilo la malalamiko namba 23627 lilifunguliwa na Paulo Kisabo na kupangwa mbele ya Hakimu Mkazi Francis Kishenyi.

Licha ya Fatma kufika mahakamani hapo leo Septemba 5, shauri liliitwa mbele ya hakimu Nyamburi Tungaraja ambaye aliliahirisha hadi Oktoba 7, 2024.

Mlalamikaji Kisabo ambaye ni wakili akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya hakimu Kishenyi kuhamishwa kituo cha kazi.

Amesema kwa sasa kesi hiyo bado haijapangiwa hakimu mwingine wa kuisikiliza.

“Huenda itakapofika Oktoba 7 mwaka huu itakuwa imeshapangiwa hakimu… Lakini leo afande amefika mahakamani,” amesema Kisabo.

Fatma alifika mahakamani na kuondoka pasipo waandishi wa habari kujua.

Kesi hiyo ilipoahirishwa Agosti 23 ilipangwa kutajwa leo Septemba 5, 2024 saa 6.30 mchana mbele ya hakimu Kishenyi.

Hata hivyo, Fatma alifika mahakamani saa 3.00 asubuhi na kesi kuahirishwa mbele ya hakimu Tungaraja.

Mmoja wa watumishi wa mahakama ambaye hakutaka kutajwa jina amesema Fatma alifika mahakamani saa 2.00 asubuhi akiwa kwenye gari na wakati wa kukaguliwa dereva wa gari hilo aliyekuwa mwanamke alionyesha kitambulisho chake ambacho kilionyesha ni askari wa Jeshi la Polisi mwenye nyota tatu.

Amesema abiria aliyekuwa kwenye gari hilo alikuwa amevaa mavazi meusi yaliyofunika uso wake, ambaye baadaye alishuka na kuingia mahakamani.

Fatma analalamikiwa akishtakiwa kwa kosa la kubaka kwa kundi kinyume cha kifungu cha sheria namba 131A (2) kinachoeleza anayewasaidia wahalifu kutenda kosa la ubakaji na yeye anahusika kwenye ubakaji wa kundi.

Wakili wa mlalamikaji, Peter Madeleka aliiomba mahakama kutoa utaratibu mwingine kwa kutoa amri ya kumkamata Fatma kwa kuwa alipata wito wa kuitwa mahakamani Agosti 22 lakini hakutokea.

Katika malalamiko, Kisabo anamlalamikia Fatma akidai ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), akidai alishiriki kuratibu na kufanikisha ubakaji wa kundi.

“Kwa kuwa ni kosa la jinai na waliokuwa wakitakiwa kutimiza wajibu wao hawakufanya hivyo, ndiyo maana na sisi tuko hapa. Tunaomba mahakama itoe hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa,” alidai Madeleka.

Aliiomba mahakama kutumia kifungu cha 130 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kumkamata Fatma anayedaiwa kuwa ni afande kwa kuwa malalamiko yao yanaangukia katika makosa ya jinai.

Hakimu Mkazi Kishenyi alisema kifungu hicho hakilazimishi mahakama kutoa amri ya kukamatwa pekee, bali pia kinatoa fursa ya kutoa hati ya wito.

“Nitatoa hati ya wito nyingine ili nijiridhishe kama hati ya wito tuliyoitoa jana (Agosti 22) haijamfikia,” alisema na kuahirisha shauri hilo hadi leo Septemba 5.

Shauri hilo la malalamiko limefunguliwa wakati ambao katika mahakama hiyo kukiwa na kesi inayoendelea kusikilizwa dhidi ya washtakiwa wanne wanaodaiwa kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti, mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam.

Kesi hiyo inayoendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa Jamhuri inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule.

Washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Jumatatu, Agosti 19, 2024 na kusomewa mashtaka ya kumbaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti huyo anayetajwa mahakamani kwa jina la XY. Baada ya kusomewa mashtaka walikana.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa faragha, washtakiwa ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.

Tayari mashahidi 12 akiwamo binti anayedaiwa kubakwa na kuingiliwa kinyume cha maumbile wameshatoa ushahidi.

Related Posts