RAFIKI yangu Kassim Liogope amepewa jukumu zito la kukaimu nafasi ya ukocha mkuu wa Azam FC muda mfupi baada ya timu hiyo kumtimua kocha Youssouph Dabo.
Kabla ya kubebeshwa mzigo huo, Liogope alikuwa akifundisha kikosi cha vijana cha Azam na alinasa kibarua hicho baada ya Dodoma Jiji aliyoitumikia msimu uliopita akiwa kocha msaidizi kuamua kutompa mkataba mpya.
Mimi binafsi sioni kama Kassim Liogope amepata fursa hiyo ya kuwa kaimu kocha mkuu wa Azam kwa bahati mbaya bali amestahili kabisa kutokana na alichokifanya huko nyuma pindi alipokuwa kocha msaidizi wa Dodoma Jiji.
Ni kocha mwenye uelewa mkubwa wa mpira wa miguu na pia ana maarifa mengi yanayohusu kazi yake ya ukocha huku na pamoja na hilo amekuwa ni mtu anayependa kujifunza mara kwa mara kwa kuhudhuria kozi mbalimbali za ukocha.
Kuhusu ufahamu wake wa soka la Bongo sina shaka naye kwani kabla hata ya kuwa kocha alishaanza kuutumikia mpira wa miguu akiwa ni mwandishi wa habari za michezo na mchambuzi katika vituo tofauti vya habari jijini Dar es Salaam.
Wakati akiwa ndio kwanza ameanza majukumu yake pale Azam ni usia wangu ambao ningependa kumpatia leo ambao kwanza ni kuishi vyema na kila mmoja anayemzunguka ndani ya timu hiyo na afungue milango ya kupokea ushauri kutoka kwa wadau na wasio wadau wa timu hiyo.
Awe pia ni mtu mwenye kusimamia taaluma yake. Asikubali kufanya mambo kinyume cha taaluma yake kwani itamfanya heshima yake ishuke na thamani yake itaporomoka pamoja na kuathiri ufanisi wake ndani ya Azam.
Akumbuke pia kuendeleza uhusiano mzuri alionao na vyombo vya habari. Ushirikiano ule ambao alikuwa anautoa wakati alipokuwa Dodoma Jiji anapaswa kuuendeleza kwa vyombo vya habari kwa vile vinaweza kumjenga au kumbomoa kutegemeana na uhusiano wake utakavyokuwa.