Aliyejinyonga akidaiwa kumbaka mjukuu wake, aacha ujumbe mke na wanawe wasimzike

Moshi. Babu anayetuhumiwa kumbaka mjukuu wake wa miaka minane na kisha kujiua kwa kujinyonga baada ya mke wake kumfuma, aliacha ujumbe kwa mkewe huyo, Philipina Olomi pamoja na watoto wake sita wasimuwekee udongo kwenye kaburi lake siku ya maziko yake.Mzee huyo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kifuni, kata ya kibosho Magharibi, Wenseslaus Ulomi (50) anadaiwa kuchukua uamuzi huo wa kujiua baada ya kubaini mkewe amefahamu alimbaka mjukuu wake huyo, anayesoma darasa la kwanza katika moja ya shule iliyopo kijijini hapo akihofia aibu na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.Septemba 3, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema lilitokea Septemba 2, 2024 na kwamba mwanaume huyo alijiua kwa kujinyonga kwa kutumia shuka ambalo alilifunga juu ya kenchi ya chumba chake.”Mnamo Septemba 2, mwaka huu huko kijiji cha Kifuni, kata ya Kibosho Magharibi Wenseslaus Olomi alibainika kujinyonga kwa kutumia shuka ambalo alilifunga juu ya kenchi ya chumba anachoishi na chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia uliosababisha mwanaume huyo kuchukua maamuzi hayo,” alisema Kamanda Maigwa.Mke wa marehemu asimulia ilivyotokea Philipina Olomi, ambaye ni mke wa Wenseslaus (marehemu), anasema Agosti 27, 2024 akiwa nyumbani kwake amelala, mumewe huyo alirudi akiwa amelewa na kumtaka aondoke nyumbani hapo. Ambapo alipoondoka hakuondoka  na wajukuu zake ndipo mwanaume huyo alipopata nafasi ya kumfanyia ukatili mjukuu wake huyo.”Jumanne iliyopita saa sita usiku, huyu baba alirudi nyumbani akiwa amelewa, nikiwa nimelala akanikimbiza, akaniambia hanitaki hapa nyumbani ataniua au yeye ajiue,” anasema.”Nikamwambia kwa nini unataka unifukuze, akaniambia nataka uondoke hapa nyumbani kwangu, nikamwambia wewe mbona kila siku huku nyumbani ni ugomvi mbona hupumziki na ninaumwa? akaniambia toka tu ili nipate amani, ukiwa hapa sina amani kabisa,” anaeleza mama huyo.Anasema hakusita kuondoka nyumbani hapo na kwamba siku hiyo wakati anataka kuondoka ndipo mumewe huyo alimvamia mjukuu wake  na kumfanyia ukatili huo na kumrubuni kwa Sh400.”Siku nyingine huwa nakimbia na wajukuu zangu lakini siku hiyo sikukimbia nao, nilipofanya naondoka ndipo mume wangu akamvamia na kumwingilia huyu mjukuu wangu akampa Sh400 akamwambia asiniambie.””Nilimchukua mtoto na kumkagua na kukuta ni kweli kaumizwa, nilishtuka sana sikujua hata nifanye nini, nimlilie nani, Ijumaa asubuhi siku iliyofuata nikatafakari niende mbele au nyuma, nikajiuliza maswali nitamwambia nini baba yake huyu mtoto, nikakosa jibu,” anasema.Anasema ilimbidi aende nyumbani kwa mama mkwe wake kumweleza jambo hilo. Ambapo mama mkwe alimtaka amtafute shangazi yake huyo mtoto ili waone cha kufanya, ambapo alimshauri pia kumuhamisha shule. Ujumbe aliouacha marehemu Mama huyo anasema baada ya kuondoka nyumbani hapo kutokana na vitisho alivyopata kwa mume wake huyo (marehemu) aliacha ujumbe kwa mtoto wa kaka yake kwamba yeye pamoja na watoto wake wasimuwekee udongo (wasimzike).”Nilipata ujumbe kwa ndugu yake (mtoto wa kaka yake) kwamba alisema akifa mimi na watoto wangu tusimwekee udongo,” anasema mama huyo.Hivyo kutokana na ujumbe huo mume wake aliouacha anasema hatashiriki maziko yake kama watu wengine na hataweka udongo kwenye kaburi lake.Akizungumzia ukatili aliofanyiwa na babu yake, mtoto huyo wa miaka minane (jina linahifadhiwa) anasema babu yake alimchukua na kumpeleka kitandani kwake na ndipo alipomfanyia ukatili huo.”Babu alinichukua na kunipeleka kulala kule kwake ndio akanifanyia hivyo na akanipa Sh400 akasema nisimwambie mtu,” anaeleza mtoto huyo.Mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake, Septemba 7, 2024.

Related Posts