Taifa Stars ilijikaba yenyewe kwa Wahabeshi

TAIFA Stars imeanza mbio za kusaka tiketi ya kwenda katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika mwakani huko Morocco, kwa kudondosha pointi mbili nyumbani mbele ya timu ya Ethiopia kwa kulazimishwa suluhu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo ya Kundi H iliyopigwa janai usiku, Stars ilishindwa kuwapa raha mashabiki waliojitokeza uwanjani kwa aina ya soka ililocheza na hasa uamuzi wa Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ na wenzake kujaza wachezaji wenye asili ya kujilinda, badala ya washambuliaji ili kutengeneza nafasi za kupata ushindi nyumbani, licha ya ukweli Ethiopia wanacheza soka la kutembeza boli na akili nyingi uwanjani.

Matokeo hayo ya suluhu nyumbani, yamevuruga kampeni za Stars kuzoa pointi tisa nyumbani, kwani sasa italazimika kushinda mechi mbili zilizosalia na pia kufanya vizuri katika michezo ya ugenini ukiwamo wa Jumanne dhidi ya Guinea ambayo leo Ijumaa inavaana na DR Congo, timu nyingine za kundi hilo.

Stars inasaka tiketi ya kucheza fainali za nne za michuano ya Afcon, baada ya zile za 1980, 2019 na mwaka huu zilizofanyika Ivory Coast na kuishia hatua ya makundi tu.

Mwanaspoti lilikuwa uwanjani kushuhudia mchezo huo dhidi ya Ethiopia na hapa chini ni dondoo za kilichoiangusha Stars ikiwa nyumbani na kazi iliyonayo kwa mechi zilizobaki za kundi hilo kama kweli inataka kwenda Morocco katika fainali za Afcon 2025.

TA!
TA!

Licha ya wengi kuamini kuwa kudondosha pointi mbili nyumbani hakuwezi kuwa sababu ya Stars kushindwa kufikia malengo, lakini ni wazi timu hiyo ina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha inapata matokeo kwenye mechi zilizobaki.

Stars ikiwa nyumbani kipindi cha kwanza imeshindwa kuonyesha ubora eneo la ushambuliaji kutokana na kushindwa kutumia nafasi chache ilizozitengeneza.

Kocha Morocco amekiri pia changamoto ya ukosefu wa umakini kwenye safu ya umaliziaji, huku akisisitiza kuwa muda bado anao kurudi kwenye uwanja wa mazoezi kufanyiwa kazi shida hiyo.

Kwenye mchezo wa juzi kocha Morocco anaweza akawa sababu ya kukosekana kwa mabao kutokana na kupanga kikosi ambacho kilikuwa na wachezaji wanane wa kujilinda na watatu tu ndio wakiwa na asili ya ushambuliaji.

Wachezaji wa asili ya ushambuliaji walikuwa ni Clement Mzize, Edwin Balua na Feisal Salum tu, huku wengine wote waliobaki wakiwa ni wa nafasi za kujilinda kuanzia kipa Ally Salim, mabeki Nickson Kibabage, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, Dickson Job, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Lusajo Mwaikenda, na viungo wa ulinzi Himid Mao Mkami na Novatus Dismas.

Kwa upangaji wa kikosi cha aina hiyo ni wazi kuwa kocha alihitaji kujilinda zaidi na sio kushambulia kama watanzania wengi walivyokuwa wanatarajia.

TA2
TA2

Kweli Ligi Kuu Bara kwa sasa eneo ambalo ni bora na linafanya kazi nzuri ni la kiungo mkabaji na mshambuliaji hilo limethibitishwa msimu uliopita mfungaji bora ametoka eneo la kiungo.

Licha ya ubora huo, kwa upande wa kikosi cha Stars ni changamoto ya kudumu kwani ni eneo ambalo limekuwa tatizo kubwa kutokana na kukosekana muunganiko mzuri ambao ungeweza kuirahisishia safu ya ushambuliaji kutokutumia nguvu nyingi kusaka nafasi za kufunga.

Stars ikikutana na timu ambayo inatumia mfumo wa kujilinda ni mtihani kwao kutokana na kukosekana kiungo mshambuliaji bora ambaye anaweza kufungua njia ili kumpa au kuwapa mwanya washambuliaji ambao na wao wamekuwa wakishuka kusaka mipira.

Ukosekanaji wa pasi za mwisho bora za kuwapa urahisi washambuliaji kupachika mabao ndio shida kubwa ya ukosekanaji wa mabao kwenye kikosi cha Stars.

Feisal Salum ‘Fei Toto’ Himid Mao na Novatus walioanza kama viungo katika mchezo huo walishindwa kuwa na kutengeneza mapishi kwa kina Balua na Mzize,  ambao walilazimika kushuka sana chini ili kusaka mipira ya kuipandisha mbele, hasa kutokana na Waethiopia kucheza soka la kumiliki mchezo na pasi nyingi.

Angalau kidogo mabadiliko ya kipindi cha pili yalileta uhai na hasa alipoingia kiungo wa ushambuliaji Mudathir Yahya, lakini bado kulikuwa na tatizo la kutotumia nafasi chache zilizopatikana kwa wachezaji wa Stars kukabana wenyewe akiwamo straika Wazir Junior ambaye hakuwa na siku nzuri akishindwa kufanya uamuzi wa haraka na kuua mashambulizi kabla hajainyima timu yake bao kwa kusimama katika njia ya shuti lililokuwa likienda wavuni la Mzize na hivyo kuikoa Ethiopia baada ya mpira huo kumgonga.

TA3
TA3

Kwenye eneo la ulinzi Stars ipo kwenye ubora wa hali ya juu ikiundwa na wachezaji ambao wamehudumu muda mrefu kwenye timu zao kwa pamoja na wamekuwa na maelewano mazuri.

Dickson Job, Ibrahim ‘Bacca’ kwa upande wa mabeki wa kati ni wachezaji ambao wamekuwa na mwendelezo wa kufanya vyema, huku pembeni nahodha wa Simba, ‘Tshabalala’ akionyesha uzoefu mkubwa na kulia Mwaikenda akihakikisha jahazi halizami.

Stars sasa ina kibarua kwa mchezo ujao dhidi ya Guinea utakaopigwa Jumanne huko Ivory Coast ambako wenyeji walichagua kuwa uwanja wa nyumbani, ili kujitengenezea mazingira mazuri kabla ya mechi za raundi zijazo zitakazopigwa mwezi ujao, ikitarajiwa kucheza nje ndani na DR Congo.

Ni vyema makocha wa Stars kuutumia mchezo wa leo saa 1:00 usiku kati ya DR Congo na Guinea kuwasoma mapema wapinzani hao kabla ya kuwafuata kwenye Uwanja wa Charles Konan Banny jijini Yamoussoukro, Ivory Coast na baada Oktoba kukutana na DR Congo kwa michezo miwili mfululizo.

TA4
TA4

Morocco alisema ameridhishwa na uwezo wa wachezaji wake ambao amekiri kuwa walikuwa bora zaidi kipindi cha pili na anaamini bado wana nafasi ya kufanya vizuri na hatimaye kufuzu kushiriki Afcon nchini Morocco.

“Mbinu niliyoitumia ya walinzi wengi ni kutokana na kuwasoma wapinzani wetu mapema kabla ya mchezo na kubaini ubora na udhiafu wao, kilichotukwamisha ni eneo la ushambuliaji.”

Related Posts