Mhadhiri UDSM ashinda ubunge EALA, awashukuru upinzani

Dodoma. Wabunge wa Tanzania wamemchagua Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Gladnes Salema kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) baada ya kupata kura 254 kati ya kura 272 zilizopigwa katika uchaguzi huo.

Uchaguzi huo umefanyika leo Alhamisi, Septemba 5, 2024 bugeni jijini Dodoma ili kujaza nafasi hiyo iliyoaachwa wazi na Dk Shingo Sedoyoka aliyefariki dunia Juni 13, 2024.

Akitangaza matokeo hayo, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amesema idadi ya wabunge wote Kikatiba katika Bunge hilo ni 393 lakini waliopiga kura walikuwa 274.

Amesema kura zilizoharibika zilikuwa ni mbili, halali ni 272, na 18 zilikuwa ni hapana.

“Sasa namtangaza rasmi Dk Gladnes Salema kuwa ndio mbunge wetu wa kuwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki,” amesema Zungu.

Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, Dk Gladnes amesema atahakikisha anaunganisha (linking) fursa zilizopo nchini ili kuifanya Tanzania kuwa Kitovu cha Uchumi wa Afrika Mashariki.

“Kwa nafasi niliyoipata nitahakikisha nchi inakwenda kunufaika kwa kupata wawekezaji kutoka mataifa, shirika na kuendelea kudumisha ushirikiano ili kujipatia fursa za ndani na nje ya nchi,” amesema.

Awali, akizungumza ndani ya Bunge alipopewa fursa na Zungu, Dk Salema amewashukuru wabunge wa upinzani kwa kile alichosema anaamini nao wanaimani na yeye.

 “Naomba nimshukuru sana Rais wangu Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini pamoja na chama changu cha Mapinduzi na viongozi wote, lakini pia naomba niwashukuru wabunge wote wa upinzani ninaamini wote wanaimani pia na mimi,” amesema Dk Salema.

Uchaguzi huo ulifuata baada ya mchujo uliofanywa na Kamati ya wabunge wa CCM, Septemba 2, 2024 baada ya Dk Salema kuwashinda wenzake wawili kwa kupata kura 161. 

Wagombea wengine wa nafasi hiyo walikuwa ni Lucia Pande (53) na Queenelizabeth Makune (52).

Uchaguzi huo ulitanguliwa na awamu ya kwanza ambapo wabunge hao walifanya uchaguzi ya kuchagua wagombea watatu kati ya kumi waliopitishwa na Kamati Kuu ya CCM.

Katika awamu ya kwanza ya uchaguzi huo, Dk Salema aliongoza kwa kupata kura 61, akifutiwa na Lucia Pande (49), Queenelizabeth Makune (44).

Wengine na kura zao katika mabano ni Fatma Kange (42), Theresia Dominic (32), Profesa Neema Kumburu (15), Fatma Msofe (7), Hawa Nkwera (5) na Maria Sebastian (4).

Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi huo, Issa Haji Gavi alisema kutofautiana kwa jumla ya idadi ya kura katika awamu hizo mbili kulitokana na baadhi ya wabunge kurejea bungeni.

Alifafanua waliopiga kura katika awamu ya kwanza walikuwa ni wabunge 269 lakini awamu ya pili walipiga kura ni 244.

Related Posts