Falsafa ya 4R kuubeba uchaguzi wa Mbeya

Mbeya. Mbeya ni miongoni mwa mikoa 26, inayotarajiwa kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ajili ya kuwapata wawakilishi wa wananchi ngazi ya vijiji, mitaa na vitongoji.

Haki, usawa na amani ndiyo misingi inayotazamwa kufanikisha uchaguzi huo kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Novemba 27, 2024, ikiwa ni hatua ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais mwaka 2025.

Mkoani humo, joto la kisiasa linazidi kupanda huku Serikali ikiweka mikakati madhubuti kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa utulivu, usawa na haki kwa washiriki wote wa uchaguzi.

Kwa mujibu wa Homera, maandalizi ya mkoa huo yanazingatia falsafa ya 4R iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inayohusisha maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi katika kuelekea kwenye uchaguzi huo, Homera anasema tayari kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ,imejipanga kusimamia uchaguzi huo kwa umakini, ili kuhakikisha unakuwa wa amani na unaozingatia kanuni za demokrasia.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi na viongozi wa vyama vya siasa ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na kwa usawa.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusisitiza sera ya 4R na sisi kama viongozi tumejipanga kuitekeleza kwa vitendo,” anasema Homera.

Mbeya ni moja ya mikoa inayoonekana kuwa na ushawishi mkubwa kwa vyama vyote vya siasa, na hivyo uchaguzi huo unatarajiwa kuwa na mvuto wa pekee.

Hali hii inafanya macho na masikio ya wengi kufuatilia kwa karibu mchakato wa uchaguzi mkoani humo.

Kwa mujibu wa Homera, uchaguzi huo utasimamiwa kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kila mgombea anapata nafasi sawa na huru ya kushiriki.

Serikali ya Mkoa wa Mbeya imejipanga kutekeleza falsafa ya 4R, inayolenga kuimarisha maridhiano, kujenga taifa lenye ustahimilivu na kuleta mabadiliko ya kweli.

Sera hii imekuwa msingi muhimu wa juhudi za kuimarisha amani na utulivu katika kipindi cha uchaguzi.

“Mbeya imekuwa tulivu kwa muda mrefu, na lengo letu ni kuhakikisha hali hii inaendelea.Tutatoa elimu kwa vyama vya siasa na wananchi kuhakikisha  uchaguzi unafanyika kwa haki na amani,” anasema Homera.

Mkuu huyo wa Mkoa anaeleza wamejipanga kutekeleza kikamilifu maelekezo na miongozo yote iliyotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Maelekezo hayo, anasema ni mabadiliko ya kanuni za uchaguzi. Hii ni pamoja na kuhakikisha vyama vyote vya siasa vinapata fursa ya kushiriki kikamilifu bila kubughudhiwa.

“Tayari tumepokea miongozo kutoka Tamisemi na maandalizi yamefikia zaidi ya asilimia 98. Tutaendelea kusimamia kwa umakini kanuni na miongozo hii ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki, na usawa,” anaongeza.

Kikao cha pamoja na vyama vya siasa

Moja ya mikakati muhimu ya kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za mitaa mkoani humo unakuwa wa amani, ni kukutanisha vyama vyote vya siasa na vyombo vya usalama ili kujadili na kuweka mikakati ya pamoja.

Homera anaeleza kikao hicho kitakuwa na lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu taratibu za uchaguzi, ili kuepusha migogoro na migongano ambayo inaweza kujitokeza.

“Kikao hicho kitahusisha viongozi wa vyama vya siasa na vyombo vya usalama, ambapo tutajadili na kuweka sawa masuala muhimu yanayohusu uchaguzi.

“Lengo ni kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu bila kuvuruga shughuli za kimaendeleo za wananchi,” anasema Homera.

Mkuu huyo  anasema uchaguzi ni haki ya kikatiba ya kila mwananchi na kufanyika kwake, hakutasimamisha shughuli za kiuchumi.

Badala yake, anasema lengo ni kuhakikisha wananchi wanatimiza haki yao ya kupiga kura na kuchagua viongozi bora watakaowaongoza katika kuleta maendeleo.

Kuchagua viongozi wenye weledi na uzalendo

Homera anavihimiza vyama vya siasa kuhakikisha vinateua wagombea wenye sifa stahiki, uzalendo na uwezo wa kuongoza kwa ufanisi.

Anasisitiza viongozi wasio na uadilifu hawapaswi kupewa nafasi katika uongozi, kwa sababu  hawatakuwa na uwezo wa kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Teknolojia imekua na wananchi wanajua ni nani kiongozi bora wa kuwaongoza. Vyama vya siasa vinapaswa kuleta wagombea wenye uzalendo, wenye uwezo wa kusimamia masuala ya maendeleo na wale wenye nia ya kweli ya kuwahudumia wananchi,” anasema.

Homera anasisitiza wananchi wa Mbeya wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi huo, kwani ni fursa muhimu ya kuchagua viongozi watakaoleta mabadiliko ya kimaendeleo.

Amani na heshima ya Mbeya

Akizungumza kuhusu umuhimu wa kudumisha amani mkoani Mbeya, Homera anasema ni dhamira ya Serikali kuhakikisha uchaguzi unafanyika bila kuathiri utulivu na heshima ya mkoa huo.

Anasisitiza vikao vya pamoja na vyama vya siasa vitakuwa na tija kubwa katika kujenga mazingira mazuri ya uchaguzi wa amani.

“Tunataka kuona uchaguzi unafanyika kwa usawa na vyama vyote vikikubaliana na matokeo bila malalamiko. Ni muhimu tukahakikisha tunalinda amani na utulivu wa Mkoa wetu,” anasema.

Kwa mujibu wa Homera, hatua za maandalizi zimefikia pazuri na Serikali inajipanga kuona kwamba vyama vyote vinakubaliana na uchaguzi na hakuna migogoro inayojitokeza. Lengo kuu ni kuhakikisha kila mwananchi anashiriki kikamilifu katika  uchaguzi huo na kwamba demokrasia inaheshimiwa.

Akizungumzia watu wa makundi maalumu, anasema kila mmoja mwenye sifa ya kupiga kura, ana haki ya msingi ya kushiriki uchaguzi huo kwa kuchagua au kuchaguliwa.

Hivyo, amesema watahakikisha wote wanapata nafasi ya kushiriki katika uchaguzi huo na watapewa kipaumbele kuhakikisha wanatimiza haki yao.

Anasema kama  ilivyo kwa Watanzania wengine wenye sifa hiyo, ni wazi hata makundi hayo yana haki kama yao, hawapaswi kubaguliwa ndiyo maana Serikali inawatambua.

Hivyo, Homera anasema watahakikisha  makundi yote yakishiriki vyema uchaguzi huo  bila usumbufu.

“Sisi kama mkoa tumejipanga kusimamia kikamilifu shughuli hii tangu mwanzo mpaka hatua ya kutangazwa washindi. Tunatamani kuona watu wote wenye sifa wakishiriki uchaguzi huu kwa sababu ndiyo chanzo cha maendeleo,” anasema Homera.

Hata hivyo, ameliomba Mwanachi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi katika kipindi hiki cha maandalizi ya kuelekea uchaguzi huo.

“Kadri muda unavyokwenda tutaendelea kutoa matangazo kuhusu uchaguzi kama Serikali inavyoelekeza, wasimamizi watatoa elimu kwa wapiga kura katika maeneo ya vituo vitakavyotangazwa.”

“Tunaomba Mwananchi muwe sehemu ya uhamasishaji kwa wananchi kushiriki uchaguzi huu na ofisi ya Mkuu wa Mkoa itatoa ushirikiano wote ili kutimiza malengo ya kitaifa,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Related Posts