Dar es Salaam. Wakati China ikitarajia kutoa msaada wa kifedha wa Sh138 trilioni (Yuan 360 bilioni) kwa mataifa ya Afrika kwa miaka mitatu, Rais Samia Suluhu Hassan amesema taifa hilo ni mshirika bora wa maendeleo kwa nchi za Afrika na kupitia jukwaa lake, mataifa hayo yatazidi kuimarisha ushirikiano huo.
Rais Samia amebainisha hayo leo Septemba 5, 2024 kwenye Jukwaa la Ushirikiano kati ya China – Afrika (FOCAC) lililofanyika jijini Beijing, China na kuhudhuriwa na wakuu wa nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika.
Serikali ya China ambayo ndiyo imeandaa mkutano huo, imeeleza kwamba iko tayari kutoa msaada wa kifedha wa Yuan 360 bilioni (Sh138 trilioni) katika miaka mitatu ijayo, zikiwemo Yuan 210 bilioni (Sh80.5 trilioni) kwa ajili ya mikopo na Yuan 80 bilioni (Sh30.6 trilioni) za misaada ya aina mbalimbali.
Pia, imebainisha kwamba itahamasisha kampuni za China kuwekeza si chini ya Yuan 70 bilioni (Sh26.8 bilioni) katika barani Afrika.
Katika hotuba yake kwenye mkutano huo, Rais Samia amesema licha ya athari zilizosababishwa na Uviko-19, China imejidhatiti katika kutekeleza iliyoahidi kwenye mkutano wa nane wa Focac hususani mipango tisa.
“China imekuwa rafiki yetu katika mapambano dhidi ya umasikini na kuleta maendeleo. Hili linadhihirika kwenye maendeleo ya miundombinu na ukuaji wa viwanda vidogo na vya kati katika mataifa yetu,” amesema.
Rais Samia amesema mpango wa Focac wa Beijing wa mwaka 2025/27 unalenga kujibu mahitaji ya mataifa ya Afrika. Amesema wakati wakipongeza mafanikio yaliyopatikana, wanapongeza kutangazwa kwa maeneo mengine ya ushirikiano katika ya China na Afrika.
Amesisitiza kwamba mpango huo utawezesha China na Afrika kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali na kiuchumi. Amesema wanapongeza, pia, uhusiano mpya wa China – Africa.
“Mkutano huu unafanyika ukiwa umepita muongo mmoja tangu Rais wa China, Xi Jinping alipotangaza mkakati wa China – Afrika jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kwanza Afrika mwaka 2013,” amebainisha Rais Samia.
Amesisitiza kwamba katika ziara hiyo, Rais Jinping alieleza kwamba kanuni za uadilifu zitatumika kama msingi wa ushirikiano kati ya China – Afrika, jambo ambalo wanaliishi hadi sasa.
“Uwepo wetu hapa leo, unaakisi mshikamano na umoja katika kujenga mustakabali wa pamoja wa maendeleo na mafanikio. Twende pamoja kuelekea mafanikio ya uvumbuzi wa kijamii na kiuchumi na maendeleo ya nchi zetu,” amesema Rais Samia kwenye mkutano huo.
Awali akifungua mkutano huo, Rais Jinping amesema Kuanzishwa kwa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika mwaka 2000 ni hatua muhimu katika historia ya uhusiano kati ya China na Afrika. Katika kipindi cha miaka 24 iliyopita, hasa baada ya enzi mpya.
“Tunasimama bega kwa bega, mkono kwa mkono, na kutetea kwa uthabiti haki na maslahi halali ya kila mmoja wetu katika mabadiliko ya karne iliyopita duniani. Katika wimbi la utandawazi wa kiuchumi, tumeimarisha misuli yetu na kuimarisha nguvu zetu.
“Tumetoa matokeo mazuri ambayo mamia ya mamilioni ya watu nchini China na Afrika wamefaidi. Katika kukabiliana na majanga makubwa na magonjwa ya mlipuko, tulifanya kazi pamoja katika hali ngumu na mbaya, na kuandika hadithi zenye kugusa moyo wa urafiki wa China na Afrika,” amesema.
Rais Jinping ameongeza kuwa baada ya karibu miaka 70 ya kazi ngumu, uhusiano kati ya China na Afrika uko katika kiwango bora katika historia. Akiangalia mustakabali, anapendekeza kwamba uhusiano wa pande mbili uboreshwe na kuwa na kiwango cha uhusiano wa kimkakati.
Kiongozi huyo amesema China na Afrika zinachukua theluthi moja ya watu wote duniani. Bila ya usasa wa China na Afrika, amesema kusingekuwa na ulimwengu wa kisasa. Ameongeza kuwa Katika miaka mitatu ijayo, China inapenda kufanya kazi na Afrika kutekeleza Mambo 10 ya Ushirikiano wa Uboreshaji wa Kisasa kati ya China na Afrika ili kuimarisha ushirikiano kati.
Kwa upande wake, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema wamekutana katika kipindi ambacho ulimwengu unakabiliana na changamoto mbalimbali kama vile mabadiliko ya tabianchi.
“Changamoto hizi zinayakumba mataifa yote lakini athari Zaidi zinaonekana katika bara la Afrika. Licha ya changamoto hizi, bado kuna fursa ya kukabiliana nazo,” amesema Rais Ramaphosa.