MCC yaanza kibabe kriketi TCA

SEPTEMBA imeanza vyema kwa timu ya MCC ya kriketi iliyoshinda kwa mikimbio 83 dhidi ya Caravans D katika mchezo wa Ligi ya TCA ya mizunguko 20 iliyopigwa jijini Dar es Salaam.

Kumzidi mpinzani kwa mikimbio 83 ni ushindi mkubwa na mashujaa walikuwa Gokul Nair aliyekuwa na mikimbio 64 na Roshan Gaussian 59 kwa washindi.

“Ni ushindi wa kishindo kwa mchezo wa kriketi kwani ni nadra tofauti kufikia zaidi ya mikimbio 80,”  alisema Ateef Salim, msemaji wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA), ambao ndiyo waandaaji wa ligi.

MCC ndiyo waliopata kura ya kuanza kubeti na wakamudu kutengeneza mikimbio 165  huku wakipoteza wiketi 6 baaada ya kutumia mizunguko 18. Mikimbio 165 ilikuwa ni mlima mrefu kwa Caravans D kuupanda, kwani jitihada zote ziligota kwenye mikimbio 82 baada ya wote kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 14.

Lakini kinyume na mechi baina ya MCC na Caravans D, Patel Titans na Union Youths haikuwa ya upande mmoja kwani ni mikimbio 17 ndiyo iliyowapa ushindi Patel Titans. Wakianza kwa kubeti, Titans walikuwa na mikimbio  118 baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko yote 20.

Baada ya kukaza msuli, Union Youths walijitahidi na kufikisha mikimbio  101 huku wakipoteza wiketi 7 hadi mwisho wa mizunguko 20 na hivyo kushindwa kwa mikimbio 17. Harsh Khidkikar aliyeiletea  Titans mikimbio 33 na Acrey Pascal aliyeongezea  24  walisaidia kuipa ushindi Titans.

Kwa Union Youths, Abhinav Sharma ambaye  aliangusha wiketi 4  za wapinzani alicheza vizuri licha ya timu yake kufungwa katika mchezo huo. Annadil Burhan  imetinga fainali ya TCA kwa mizunguko 30.

Related Posts