Hai. Balozi wa Utalii Tanzania, Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo anatarajia kuanza safari ya siku saba ya kuupanda Mlima Kilimanjaro kesho Septemba 6, 2024 huku akiwataka Watanzania kujenga tabia ya kutembelea vivutio vilivyopo nchini ikiwemo kupanda mlima huo mrefu barani Afrika, hatua itakayochochea utalii wa ndani.
Bongo Zozo ameyasema hayo leo Septemba 5, 2024 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) baada ya kuwasili kwa ajili ya kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuhamasisha utalii wa ndani.
Balozi huyo ambaye atapanda mlima huo na kundi la watu 47 kutoka Kikundi cha Kili Summiters, amesema Watanzania wana wajibu wa kupenda vya kwao na kuhakikisha wanapanda Mlima Kilimanjaro ili kujionea maajabu ya Mungu.
“Hii ni mara yangu ya tatu kupanda mlima huu na nitaanza safari ya siku saba ya kuupanda kesho Septemba 6, 2024. Hakika kupanda Mlima Kilimanjaro ni mazoezi ya misuli, mwili na roho, hivyo kila Mtanzania anapaswa kuupanda ili kushuhudia uzuri wake.
Ameongeza kuwa: “Mimi kama balozi wa utalii napenda sana kuutangaza utalii, nitoe wito kwa Watanzania, waone Mlima Kilimanjaro kama wa kwao, ni mali yao na si mali ya watalii kutoka nje. Ni sawa unaingiza hela ya utalii lakini ni mali yenu, oneni ni wajibu wenu kuupanda na kuutangaza.”
Kiongozi wa kikundi cha Kili Summiters, Makuliro Kassera amesema huu ni mwaka wa tano tangu kundi hilo lilipoanza kupanda Mlima Kilimanjaro na kwamba kwa mwaka huu watapanda watu zaidi ya 47.
Amesema katika kipindi hicho cha miaka mitano zaidi ya watu 250 wamepanda mlima huo na mwaka huu katika kutimiza miaka mitano, wamemualika Bongo Zozo ili kuweka hamasa zaidi kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kupanda mlima huo mrefu barani Afrika.
“Tunaalika Watanzania wote na hata wananchi wa Afrika Mashariki kuupanda mlima huu, Bongo Zozo amesema hii ni zawadi yetu kutoka kwa Mungu, ni mlima wetu tuupande na kushuhudia upekee wake,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Tangu tuanze kupanda mlima huu, kila mwaka watu wanaopanda wanabadilika na mwaka huu tutatumia njia tatu, kuna watakaopita njia ya Rongai, wengine Umbwe na wengine Machame, lakini siku ya tatu tutakutana huko juu na kuungana kwa pamoja kwenda hadi kileleni.”