UONGOZI wa Dodoma Jiji umechagua kuutumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara kwa michezo ya nyumbani, baada ya Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kufungiwa na Bodi ya Ligi (TPLB) kutokana na kutokidhi vigezo.
Timu hiyo iliyoanza msimu huu bila ya kuonja ladha ya ushindi katika michezo miwili iliyocheza, ilichapwa bao 1-0 na Mashujaa kisha kulazimishwa suluhu na Pamba Jiji, itautumia uwanja huo kuanzia mechi na Namungo inayotarajiwa kupigwa Septemba 12.
Ofisa Habari wa Dodoma Jiji, Patrick Semindu aliliambia Mwanaspoti, wamechagua uwanja huo kwa ajili ya michezo ya nyumbani ingawa baada ya mechi yao na Namungo wanaamini Uwanja wa Jamhuri utakuwa tayari hivyo watarudi tena Dodoma kucheza hapo ikiwamo dhidi ya Simba itakayopigwa Septemba 29.
“Ni kweli tumechagua uwanja wa Kwaraa na malengo yetu ni kucheza mechi na Namungo tu, kisha baada ya hapo tutarudi tena Dodoma, kwa sababu wataalamu wetu wanaendelea kuyafanyia marekebisho tuliyoagizwa ambayo sio makubwa sana,” alisema.
Kwa upande wa kocha mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime alisema, wanaendelea na maandalizi kwa ajili ya mchezo huo huku wakitambua wana jukumu nzito lililokuwa mbele yao japo shauku yao ni kuhakikisha wanarejesha furaha kwa mashabiki zao.
“Tunaenda kukutana na timu ambayo pia inahitaji ushindi kama ilivyokuwa pia kwetu, tuko tayari kukabiliana na changamoto hiyo, jambo nzuri kwetu hali ya wachezaji wote ni nzuri hivyo tunaombea iwe hadi siku ya mchezo husika,” alisema Maxime.
Dodoma Jiji itakutana na Namungo ambayo nayo itaingia katika mchezo huo ikikumbwa na jinamizi la matokeo mabaya baada ya kupoteza mechi zote mbili ilizocheza hadi sasa, ikichapwa mabao 2-1 na Tabora United kisha 2-0, mbele ya Fountain Gate.
Katika michezo miwili iliyopita baina ya timu hizo msimu uliopita, Namungo iliibuka mbabe baada ya kushinda kwa bao 1-0, ikiwa kwenye Uwanja wa Majaliwa Lindi Desemba 3, 2023, huku marudiano zikitoka suluhu kwenye Uwanja wa Jamhuri Mei 14, 2024.