KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Paul Nkata amekaribishwa katika Ligi Kuu Bara kwa vipigo akipoteza michezo miwili za awali za ligi ya msimu huo mbele ya Singida Black Stars na Yanga na kumvuruga kocha huyo Mganda, akitaja sababu ni kuzidiwa ubora na kukyutana na timu hizo akiwa bado hajajipanga vyema.
Kocha huyo wa zamani wa Villa SC na Express za Uganda alichukua mikoba iliyoachwa wazi na Fredy Felix ‘Minziro’€aliyemaliza mkataba na klabu hiyo na alipokelewa na kipigio cha bao 1-0 kutoka kwa Singida kabla ya kulala 2-0 siku chache baada kutoka kwa watetezi Yanga mechi zikichezwa Uwanja wa Kaitaba.
Kupoteza mechi mbili mfululizo nyumbani, huku akikabiliwa na mechi ngumu ya kwanza ugenini dhidi ya Tabora United itakayopigwa wiki ijato imemfanya kocha huyo kuanza kulipanga jeshi upya, lakini akikiri kuanza vibaya kumemchanganya mno na sasa hataki tena kuendelea kugawa pointi katika ligi hiyo.
Timu hiyo itacheza mchezo wa tatu, Septemba 11 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora ikipigwa kuanzia saa 8:00 mchana na kocha Nkata atakayekiongoza kikosi hicho kesho katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Geita Gold mjini Geita katika kujiweka fiti aliliambia Mwanaspoti wanafanya kila kitu kuhakikisha hawapotezi mchezo wa tatu dhidi ya Tabora.
“Tulipoteza mechi ya kwanza dhidi ya Singida yenye kikosi kizuri na wachezaji wengi wa kimataifa, mechi ya pili dhidi ya Yanga ni wazi kila mtu anafahamu ubora walionao hapa Tanzania na soka wanalocheeza. Hivyo tulicheza mechi mbili ngumu, lakini tulijaribu kadri ya uwezo wetu,” alisema Nkata na kuongeza;
“Naamini tukikutana na timu ya kiwango chetu tuna uhakika wa kupata matokeo mazuri, tunajiandaa vyema na tunatumia haya mapumziko kujiimarisha ili kuwa na timu nzuri na tunatarajia kwamba ligi ikirejea tutaanza kupata ushindi.”
Nkata alisema kwa mechi ya tatu na ya kwanza ugenini, hataki tena utani wa kupoteza pointi tatu nyingine na kwamba wanaendelea kufanya maandalizi mazuri yanayompa imani ya kufanya vizuri.
“Najaribu kupambana kuhakikisha natengeneza timu ya ushindi nina imani tutafanya vizuri na kuwa kwenye malengo ya klabu,”€ alisema kocha huyo.