Babati. Dereva wa lori la mizigo linalosafiri kwenda nje ya nchi anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara kwa tuhuma za kumpiga na kitu kizito dereva wa basi la Mtei na kusababisha kifo chake.
Dereva huyo wa lori anadaiwa kumshambulia dereva wa basi hilo la abiria kwa kile kinachodhaniwa kuwa ni baada ya kumgusa maarufu kupiga pasi wakati akijaribu kumpita.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani amebainisha hayo leo Septemba 5, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo lililotokea Septemba 2, 2024.
Kamanda Makarani amesema tukio hilo la dereva huyo kujeruhiwa kisha kufariki dunia limetokea kwenye eneo la Halla mjini Babati ambapo chanzo ni dereva wa lori kumshambulia dereva wa basi na kitu butu kichwani na kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini.
Amesema awali kulikuwa na sintofahamu juu ya mgororo wa kupitana kwenye barabara baina ya madereva hao wawili wa lori na basi.
Amebainisha kwamba dereva wa lori Gasper Roman (25), mkazi wa Dodoma, akiwa na utingo wake Fabris Jema (25), raia wa Rwanda alishuka kwenye gari na kumfuata dereva wa basi, Idd Salehe (43) na kuzozana naye.
Amesema mwenye basi alikuwa nyuma ya mwenye lori na katika kumpita kukatokea sintofahamu hiyo.
“Dereva wa lori, Roman alimfuata na kumshusha garini dereva wa basi, Salehe na kumpiga kwenye kichwa kwa kutumia chuma na kumjeruhi,” amesema.
Amesema baada ya tukio hilo, dereva wa lori na utingo wake walifikishwa polisi na dereva akapelekwa hospitali na kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu.
“Tunawashikilia dereva wa lori na utingo wake kwa uchunguzi zaidi wa tukio hilo na tunatarajia kuwapeleka mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika,” amesema.
Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesikitishwa na tukio hilo la dereva wa lori kutumia nguvu kubwa wakati akizozana na dereva wa basi.
Mkazi wa Babati, Steven John amesema ameona video ikisambaa mitandaoni kwa dereva huyo wa basi kupigwa kichwani na dereva wa lori.
“Hata kama aligongwa kidogo wakati akipitwa, huyo dereva wa lori hakupaswa kumpiga kichwani dereva mwenzake hadi kusababisha kifo chake,” amesema.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.