Dar es Salaam. Kauli za hivi karibuni zinazotolewa na baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu uchaguzi na matumizi ya vyombo vya dola zinaonekana kukitesa chama hicho, kikilazimika kutoka hadharani kila mara kuzikanusha na kujitenga nazo.
Miongoni mwa kauli hizo ni iliyotolewa karibuni na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Marco Ng’umbi, aliyewakumbusha madiwani kuhusu uchaguzi wa mwaka 2020 kuwa wilayani humo kazi yote ilifanywa na Serikali kuhakikisha wanapita bila kupingwa.
Kauli hiyo imetonesha kidonda cha nyingine yenye utata na kuashiria kutokuwepo uchaguzi huru na haki, iliyokanushwa pia na CCM, ya aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kuwa ushindi si lazioma upatikane kwenye sanduku la kura, bali kuna njia nyingine za halali, nusu halali na haramu.
Pia ipo ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Faris Buruhan kwamba wanaotukana viongozi wakipotea polisi wasiwatafute.
Kauli hizo zimezua mjadala miongoni mwa wananchi hususani baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikipigania mfumo huru wa uchaguzi.
Kauli hiyo kwa nyakati tofauti zimejibiwa na viongozi wakuu wa CCM na wengine wametenguliwa nyadhifa zao na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM.
Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 5, 2024 kuhusu kauli hizo na hatua zilizochukuliwa, Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohamed Bakari amesema hatua ya CCM kujibu kauli hizo ni sehemu ya propaganda, lakini ukweli wanaujua.
“Moja ya kazi ya chama ni propaganda, sasa inapotokea mmoja wa wanachama wenu akatoa kauli ambayo inaharibu sura ya chama, mnawajibika kutoka hadharani kujitenga na kauli hiyo.
“Lakini pamoja na kukanusha, chama hakikani zile kauli kwamba zinaakisi uhalisia wa mambo yenyewe. Ukiangalia mwenendo wa siasa za Tanzania, zile kauli zinaakisi hali halisi jinsi siasa zinazofanyika nchini, kwa sababu hayo mambo huwa yanaonekana wakati wa uchaguzi,” amesema.
Amesema ili kuwe na uchaguzi ulio huru na wa haki, kuna haja ya kubadilisha Katiba na sheria za uchaguzi.
“Unapokuwa na Katiba ya msingi wa chama kimoja, unapokuwa na Tume ya Uchaguzi ya chama kimoja na vyombo vya ulinzi na usalama, ambavyo utamaduni wake ni wa chama kimoja, huwezi kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki.
“Ni lazima kuwe na mabadiliko ya Katiba na sheria na mabadiliko ya kitabia ya watu walio katika vyombo hivyo,” amesema.
Mbali na Profesa Bakari wachambuzi wengine wa masuala ya siasa na jamii, wameitaka Serikali kuwachukulia hatua makada hao kwa kuwa kauli zao zinaashiria vitendo vya uhalifu.
Mwanasheria nguli, Dk Onesmo Kyauke amesema ili uchaguzi uwe huru na wa haki, lazima sheria zitende haki.
“Hawa makada wanasema ukweli ambao haupaswi kuwekwa wazi. Tunapaswa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, hii INEC siyo huru, hata uchaguzi wa serikali za mitaa usisimamiwe na wizara.
“Hata huyo DC wamemsimamisha bure. Mtu anaposema walishiriki kuhakikisha chama kinashinda, hata ukikemea bila kubadilisha sheria itasaidia nini? Ni sawa na umwambie mtoto nenda kaibe kwa jirani, akileta unakula, halafu akisema unamkemea?” amesema.
Hata Dk Hellen Kijo-Bisimba, mwanaharakati na mwanasheria mkongwe amepita mlemle, amesema haikupaswa kuishia kwa CCM kukanusha kauli na kuwakemea tu wale makada.
“Hilo ni suala la mamlaka zinazosimamia masuala ya sheria na haki katika nchi, kwa sababu kauli nyingine ukizifuatilia ni za kihalifu, kwa mfano mtu anaposema watateka watu.
“Hata Nape alipotoa kauli ile, haikupaswa kuishia kumtengua tu, kwa sababu mambo yale yanavunja sheria, haiwezekani mseme mnafanya mbinu zisizo halali halafu mnaachwa,” amesema.
“Hizi kauli zina chembechembe kali za uvunjifu wa sheria. Suala siyo kukemewa tu, bali ni mamlaka kuwakamata na kuwafanyia uchunguzi ili hatua za kisheria zichukuliwe.
“Kauli hizi zinatufanya sisi wananchi tukose imani na uchaguzi kwa sababu hauna maana kwa kauli hizi. Watu wakishavimbiwa lazima watabeua, ndiyo maana ya kauli hizi,” amesema.
Kwa upande wake Bob Wangwe, mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) amesema:
“Kumekuwa na shida kwa CCM kukataa kauli hizi za kihalifu kwa maneno badala ya vitendo, wanafanya kwa maneno ili kuhadaa umma, wakati ni vitendo ambavyo hatua za kisheria zinapaswa kuchukuliwa,” amesema.
Amesema hata vyombo vya ulinzi na usalama vina wajibu wa kuchukua hatua.
“Zile kauli zinaashiria makosa ya jinai, kwa hiyo tulitarajia vyombo vya sheria vingechukua hatua, pengine kwa sababu ni watu wanaotokana na chama kinachoongoza Serikali,” amesema.
“Kwa DC kutenguliwa tu hakutoshi, tungetarajia vyombo vya ulinzi na usalama vingemhoji kwa sababu kumekuwa na matukio ya watu kupotea na kutekwa, lakini hatujaona.
“Serikali haijatoa tamko lolote, maana yake ni kwamba kama yule DC angenyamaza asingetenguliwa, hivyo haijulikani kwamba ametenguliwa kwa sababu alifanya vitendo viovu au ni kwa sababu ametoa siri,” amesema.
Akizungumza kupitia video iliyosambaa mitandaoni Septemba mosi, 2024, Ng’umbi ambaye uteuzi wake ulitenguliwa siku hiyohiyo, alidai Serikali iliwezesha ushindi wa madiwani na baadhi ya wabunge katika uchaguzi wa mwaka 2020.
“Sasa yale mazingira ya mwaka 2020 siyo kwamba yalikuja yenyewe automatically kwa sababu ninyi mlikuwa wagombea bora sana. Ni mazingira ambayo yalikuwa yametengenezwa na Serikali na Serikali ndiyo iliyoifanya kazi ile ya wewe kupita bila kupingwa,” alisema.
Alibainisha kuwapo matukio aliyoita ya porini bila kufafanua.
Kauli hiyo ndiyo ilimwibua Amos Makalla, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo alipoizungumza na viongozi wa CCM na Serikali wa Mkoa wa Arusha Septemba 4, 2024, na kusema chama hicho hakiwezi kubebwa na hakitegemei mbeleko katika chaguzi.
“Alisema sijui machakani, mimi nasema yule aliishiwa hotuba, akaanza kutafuta maneno yake, sie (CCM) hayatuhusu na hizo ni habari zake, yaani ilikuwa mazungumzo baada ya habari,” alisema.
“Mimi ndiyo msemaji wa CCM, tunawahakikishia Watanzania, chama hiki kimejiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani na tutashinda, hatuwezi kwenda porini kuzurura kwa sababu tuna muundo mzuri kuanzia ngazi ya kata na tuna ilani nzuri, hatuhitaji mbeleko,” alisema.
CCM pia ilijitokeza hadharani kujibu kauli ya Nape aliyesema matokeo ya kura siyo lazima yawe yale ya kwenye boksi aliyoitoa Julai 15, 2024 alipotembelea soko la Kashai mkoani Kagera na kuzungumza na wananchi akimhakikishia ushindi mbunge wa Bukoba Mjini, Stephen Byabato.
Julai 16, 2024 Makalla alisema: “Kuna kiongozi nimemsikia huko mitandaoni anasema eti ushindi wa uchaguzi hautokani na kura za kwenye boksi, mimi nataka nimwambie hiyo kauli isitazamwe kuwa inatokana na CCM.”
Alisema chama hicho kitaheshimu matokeo yoyote na uamuzi wowote wa wananchi kupitia sanduku la kura.
Aprili 17, 2024 wilayani Ngara mkoani Kagera, Mwenyekiti wa UVCCM mkoani humo, Faris Buruhan akiwaonya wanaotukana viongozi alisema:
“Kama kuna mtu anadhani, anao uhuru wa kukaa mitandaoni na kisimu chake anashinda asubuhi kutwa nzima anatukana viongozi, Jeshi la Polisi, hawa tukiwapoteza msiwatafute hawa. Piga makofi kwa CCM. Hivi wewe unajua gharama za kuwapata viongozi?”
Kauli hiyo ilikosolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi alipohutubia mkutano wa hadhara jijini Mbeya Aprili 18, 2024.
“Leo akiinuka kijana wa CCM kwa mfano, akasema wapinzani wetu wakifanya hivi na hivi lazima tuwapoteze, huyu ni kijana wetu lakini kasema jambo la kijinga, tutalipinga na lazima tuone ni la kijinga. Kwa sababu nchi hii ni yetu sote.”
Dk Nchimbi pia alikosoa kauli ya kada wa CCM ambaye hakutambulika jina wala mahali alipokuwa, aliyezungumza kupitia video iliyosambaa mitandaoni Julai 10, 2024 akitoa kauli iliyoashiria ubaguzi kwa misingi ya vyama.
Dk Nchimbi akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji na viongozi wa UVCCM ngazi za mikoa na wilaya zote, Ihemi mkoani Iringa Julai 11, 2024 aliwaonya kuepuka kutoa kauli au kufanya vitendo vyenye taswira inayoweza kutafsiriwa kuwa baadhi yao wanashabikia ukandamizaji wa haki za wananchi.
“Kama kuna jambo tunapaswa kulilinda kwa wivu mkubwa ni taswira chanya ya CCM, hasa jambo linalohusu dhamana ya kuongoza nchi yetu na kuwatumikia wananchi kwa haki na usawa, kwa kupinga kauli na vitendo vya ubaguzi na dhuluma kwa Watanzania,” alisema.