TADB yakopesha vikundi ng’ombe 153 wa maziwa

Pemba. Ili kukabiliana na changamoto ya kukosa maziwa na kuimarisha lishe, vikundi saba vya vya ufugaji vimepewa ng’ombe 153 kuwezesha sekta ya maziwa kukua.

Ng’ombe hao wenye thamani ya Sh800 milioni wamenunuliwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kutoka Afrika Kusini.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa ng’ombe hao leo Septemba 5, 2024 baadhi ya wafugaji katika wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba wamesema mbali na kuimarisha upatikanaji wa maziwa, mifugo hiyo itaboresha vipato vyao.

Mwenyekiti wa kikundi cha ufugaji cha Tupo imara, Omar Isamil Hemed amesema ng’ombe hao wa kisasa wana uwezo mkubwa wa kuzalisha maziwa, hivyo watawasaidia kumudu gharama za maisha ikiwemo kuwalipia ada watoto.

“Kabla ya kukabidhiwa ng’ombe hawa tulikuwa tunafuga wa kienyeji ambao hawana uwezo wa kuzalisha maziwa mengi,” amesema.

Ng’ombe hao imeelezwa watakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 400 za maziwa kwa siku.

Katibu wa kikundi hicho, Aminia Khamis Faki amesema waliomba ng’ombe hao kwa ajili ya kubadilisha maisha yao kutokana na hali duni walionayo.

“Tunaishukuru Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa kutupatia mkopo wa ng’ombe, tunaamini tutaondokana na hali ngumu ya maisha tulionayo. Tunaahidi ng’ombe hawa tutawatunza ili tutimize malengo yetu na kurejesha mkopo,” amesema.

Awali, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar, Asha Zahran Mohamed amesema endapo ng’ombe hao waliokabidhiwa kwa wafugaji watapatiwa malisho bora na kuimarika zaidi watasaidia kuondoa changamoto ya uhaba na upatikanaji wa maziwa kisiwani humo.

Bila kutaja kiasi, amesema Zanzibar imekabiliwa na changamoto ya upungufu wa maziwa.

“Zanzibar tuna changamoto ya uhaba wa maziwa, tuna watu wengi ambao wanahitaji maziwa, ujio wa ng’ombe hao utaondosha changamoto na kuepuka kununua maziwa kutoka nje ya visiwa hivi,” amesema.

Meneja wa ufuatiliaji na tathimini TADB, Damas Damian amesema lengo la benki hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali kuwakomboa wafugaji ili wafuge kwa tija badala ya mazoea.

Amesema hatua hiyo imefikiwa kutokana na kauli ya Wizara ya Kilimo Zanzibar juu ya upungufu wa kiwango cha uzalishaji maziwa.

Amesema benki ilinunua ng’ombe hao 153 kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kuwakopesha wafugaji.

Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji Zanzibar, Shamata Shaame Khamis amewataka watendaji wa wizara kufuatilia kwa karibu maendeleo ya wafugaji hao na kutatua changamoto zote ambazo zinaweza kujitokeza.

Related Posts