Rais wa Kenya, William Ruto, ameonyesha masikitiko yake makubwa kutokana na moto uliotokea katika Shule ya Msingi ya Hillside Endarasha, ambapo wanafunzi 17 wamepoteza maisha. Akizungumza kupitia mitandao ya kijamii, Rais Ruto ameeleza kuwa habari za tukio hilo ni “mbaya sana” na ameagiza mamlaka kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha moto huo.
“Tunawaombea manusura wapone haraka,” alisema Rais Ruto. “Naagiza mamlaka husika kuchunguza kwa kina tukio hili la kutisha, na waliohusika watachukuliwa hatua.”
Serikali ya Kenya, kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani na Uratibu wa Serikali ya Kitaifa, imeeleza kuwa inakusanya rasilimali zote muhimu ili kusaidia familia zilizoathiriwa na janga hili. Kundi la wachunguzi tayari limetumwa shuleni hapo kwa ajili ya kuanza uchunguzi wa kina, kwa mujibu wa taarifa za polisi.
Msemaji wa polisi, Resila Onyango, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa miili iliyookotwa imechomeka kiasi cha kutoweza kutambulika. “Miili zaidi inaweza kupatikana iwapo eneo hilo litachunguzwa kikamilifu,” aliongeza.
Hadi sasa, chanzo cha moto huo hakijajulikana, lakini Rais Ruto ametaja tukio hilo kuwa la “kutisha” na “la kuangamiza,” huku akisisitiza kuwa uchunguzi wa kina utawezesha kubaini waliohusika na kuhakikisha wanachukuliwa hatua stahiki.
#KonceptTvUpdates