Mbowe kumburuza Mchungaji Msigwa kortini, mwenyewe ajibu

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amevunja ukimya na kutangaza kusudio la kumfikisha mahakamani kutokana na kauli za mfululizo zinazotolewa dhidi yake na mbunge wa zamani wa Iringa Mjini kupitia Chadema, Mchungaji Peter Msigwa.

Mbowe ametangaza kusudio hilo kupitia barua ya notisi ya madai aliyomwandikia Mchungaji Msigwa kupitia jopo la mawakili watano – John Mally, Jonathana Mndeme, Hekima Mwasipu, Simon Mrutu na Dickson Matata.

Kwa notisi hiyo, amesema iwapo hatatekeleza masharti aliyompa ndani ya siku tano tangu kupata barua hiyo, atamfikisha mahakamani kutokana na kauli ambazo Mbowe anadai ni kashfa zenye lengo la kumshushia hadhi aliyoijenga kwa miaka mingi ndani na nchi na kimataifa.

Masharti ndani ya notisi hiyo ni kumtaka Mchungaji Msigwa kuchapisha taarifa katika kurasa za mbele za magazeti mawili (moja linalosambazwa kitaifa na lingine linalosambazwa kikanda), kwa namna na uzito sawa na kauli hizo, anazodai ni za uongo, ambazo amekuwa akizitoa dhidi yake katika vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na maeneo mbalimbali.

Katika taarifa atakazochapisha, Mbowe anamtaka Mchungaji Msigwa akiri na kuomba radhi kwa umma kwa kuchapisha habari za uongo kwa makusudi dhidi yake (akimtaja Mbowe kwa jina kamili).

Mchungaji Msigwa pia anatakiwa katika taarifa atakazochapisha akiri na kuomba radhi, aahidi kwa Watanzania kuwa mkweli katika maneno yake yote na kutotumia vibaya nafasi yake ya kisiasa.

“Zaidi tuna maelekezo kwamba, tunakutaka umlipe mteja wetu jumla ya Sh5 bilioni,” inasomeka sehemu ya hitimisho la notisi hiyo.

Inaelezwa na Mbowe katika notisi hiyo kuwa malipo yanajumuisha fidia ya madhara maalumu, mahsusi na ya adhabu.

Wakili Mwasipu amelithibitishia Mwananchi kuwa tayari wamempatia Mchungaji Msigwa notisi hiyo iliyoandikwa Septemba 2, 2024 na amesaini kukiri kuipokea.

Mchungaji Msigwa alijiondoa uanachama wa Chadema Juni 30, 2024 na kuhamia CCM.

Tangu wakati huo amekuwa akitoa kauli kinzani dhidi ya Chadema na Mbowe katika majukwaa ya kisiasa na kwenye vyombo vya habari.

Amekuwa akieleza namna mambo yasivyo sawa ndani ya chama hicho, pamoja na mambo mengine akimtuhumu Mbowe kuwa amekifanya kama Saccos, ameunda taasisi ya Mbowe anakopitisha fedha za chama na kwamba hataki mtu mwingine agombee uenyekiti wa chama hicho.

Alichokisema Mchungaji Msigwa

Akizungumzia notisi ya mawakili wa Mbowe iliyoelekezwa kwake, Mchungaji Msigwa amekiri kupokea notisi hiyo na kuitia saini.

Hata hivyo, amesema anamkumbusha Mbowe kwamba “matatizo ya kisiasa yanatatuliwa kisiasa.”

Amesema Mbowe amekuwa mstari wa mbele kuisema Serikali ya CCM na Rais Samia Suluhu Hassan lakini yeye ameguswa pale alipomtaka azungumzie tuhuma kadhaa ndani ya chama chake.

“Niliuliza maswali nikasema Chadema Digital ni ya Chadema? Si angejibu tu aseme ni ya Chadema, ilisajiliwa mwaka fulani…nimeuliza, wewe unapanda magari 10, mwenzako ana gari moja, si atoke hadharani ajibu?” amesema.

Amesisitiza kwamba kujaribu kumpeleka mahakamani ni kujaribu kutaka kumnyamazisha na kumtisha, kitu ambacho hawezi kutishika kwa sababu ana mambo mengi

“Mbaya zaidi, yale mambo ya mashamba na matrekta, mbona hajayaweka kwenye demand notice? Kinachonipa ujasiri ni kwamba anajaribu kutisha watu wasimseme wakati yeye anaisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Msigwa.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba yuko tayari kukabiliana na kiongozi huyo wa Chadema na hivyo akamtaka wakutane mahakamani.

Related Posts