Dodoma. Mama na mtoto wake wa kike, wakazi wa mtaa wa Muungano jijini Dodoma, wameuawa baada ya kufanyiwa vitendo vya ukatili na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo Septemba 6, 2024.
Waliouawa ni Mwamvita Mwakibasi (33) na binti yake Salma Ramadhan (13), mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Mkonze, jijini Dodoma.
Dada wa marehemu, Pendo Mwakibasi, ameeleza kuwa alipigiwa simu na mama yao mzazi kutoka Mbeya saa 8:00 usiku wa kuamkia leo, akiambiwa kuwa mdogo wake amevamiwa nyumbani kwake.
Alipofika nyumbani hapo, aliwakuta mdogo wake na mtoto wake wakiwa katika hali mbaya, wakitokwa damu sehemu mbalimbali za miili yao na wakiwa hawawezi kuongea.
Amesema waliwapeleka hospitali, lakini alihisi mdogo wake tayari alikuwa amefariki. Salma aliwekewa oksijeni na dripu, lakini baadaye wote wawili walifariki dunia.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Dodoma, Daniel Dendarugaho, amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakati uchunguzi ukiendelea.