Wydad Casablanca bado yamganda Mzize 

MIAMBA ya soka la Morocco, Wydad Casablanca imeonyesha kuwa siriazi kuitaka huduma ya mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize ambaye ni mfungaji bora wa Kombe la FA msimu uliopita.

Mzize mwenye umri wa miaka 20, ambaye ni zao la timu za vijana za Yanga, amekuwa akivutia klabu kadhaa barani Afrika, huku Wydad na Kaizer Chiefs ya Sauzi zikiwa miongoni mwa zinazomfuatilia kwa karibu.

Wydad itaongeza ofa mara tano ya ile ambayo iliripotiwa awali iliyokuwa Dola 100,000 (zaidi ya Sh271 milioni)ambazo Wananchi walizikataa.

Taarifa kutoka Morocco zinasema vigogo hao wapo tayari kutoa Dola 510,000 (zaidi ya Sh1.38 bilioni) pamoja na fursa kwa timu hiyo kwenda Morocco msimu ujao wakati wa maandalizi (Pre-season), huku gharama zote wakizibeba na watakuwa tayari kuja nchini katika tamasha lijalo la Wiki ya Mwananchi.

Pamoja na kwamba msimu mpya wa Ligi Kuu Morocco (Batola Pro) umeanza, vigogo hao wanahaha kuhakikisha wanaboresha eneo  la ushambuliaji ambalo linaonekana kuwa na upungufu tangu wakati wakianza maandalizi na pia ni pendekezo la kocha wa kikosi hicho, Rhulani Mokwena ni Mzize.  

Mzize amekuwa akiendelea kung’ara na tayari amefunga mabao mawili katika mechi za awali za hatua ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’o na moja katika ligi dhidi ya Kagera Sugar.

Kwa taarifa kutoka Morocco, Wydad imejaribu mara kadhaa kumpeleka Mzize Morocco, lakini ofa za awali zilikataliwa.

Hata hivyo, rais wa klabu hiyo, Hicham Ait Menna anaendelea na juhudi za kumsajili mchezaji huyo, licha ya msimamo wa rais wa Yanga, Hersi Said kwamba hauuzwi kwa sasa. Wydad inasubiri jibu kutoka Yanga juu ya ofa ya hivi karibuni.

Akizungumzia namna amekuwa akihusishwa na klabu kubwa Afrika, Mzize alisema: “Timu zote zilizotuma ofa ni kubwa kitendo cha kuonyesha zinanihitaji kinanifanya kuwa na shauku ya kutaka kuonyesha zaidi.”

Licha ya Wydad kuboresha ofa ugumu wa dili unachochewa na kufungwa kwa dirisha la usajili Bara, hivyo kocha wa Yanga, Miguel Gamondi atakuwa na wakati mgumu kupata mbadala wake kutokana na msimu wa mashindano kuanza.

Related Posts