Dar es Salaam. Wajasiriamali nchini wamepewaa mbinu za kuwawezesha kulifikia kikamilifu soko la ndani na nje ya nchi, wakitakiwa kuwa wabunifu wa vifungashio na mikebe ya bidhaa zao.
Maarifa hayo yametolewa leo Septemba 5, 2024 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Godfrey Nyaisa alipofungua kikao cha mashauriano na wadau kuhusu Mkataba wa Sheria ya Kimataifa ya Shirika Bunifu Duniani (Wipo), uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Nyaisa amesema kwa sasa kuna ushindani mkubwa wa kibiashara nchini na nje ya mipaka ya nchi, hasa katika kuongeza ubora wa bidhaa au huduma na mwonekano unaovutia wa bidhaa.
Amesema moja ya changamoto kubwa kwenye bidhaa, hasa zile za wajasiriamali, ni kukosa ubunifu kwenye vifungashio na mikebe ya bidhaa zao, jambo linalowakwamisha wengi.
“Nikitoa mfano mdogo na wa haraka, kwenye bidhaa za mafuta ya alizeti na asali, njia ya kutoka Dar es Salaam mpaka Singida, wajasiriamali wengi wanatumia vifungashio vya chupa za maji na madumu yaliyokwishatumika kufungashia au kuhifadhia mafuta yenye ubora ya alizeti au asali,” amesema.
Amesema changamoto hiyo hufanya wanunuzi kudhani bidhaa hizo hazina ubora au ni hafifu, kumbe tatizo lipo kwenye vifungashio na mikebe.
Hivyo amewashauri wajasiriamali hao kuhakikisha bidhaa pamoja na vifungashio au mikebe ya bidhaa vinakuwa na ubunifu wa kipekee, wenye kuvutia wanunuzi kwa kuwa hilo litasaidia kuongeza thamani na kuweka urahisi wa kuuzika kwenye bidhaa.
Pia wamehimizwa wanapofanya bunifu hizo wazisajili ili maumbo au michoro bunifu iweze kulindwa kwa mujibu wa sheria ya nchi.
“Sisi kama Brela tunaendelea na mkakati wetu wa kutoa elimu kwa wajasiriamali na wabunifu nchini ili waweze kufanya bunifu zitakazowawezesha kutambulika kirahisi sokoni na kuhimili ushindani katika masoko ya ndani na ya nje,” amesema.
Amesema mchakato ulishaanza wa kutunga Sheria ya Miliki Bunifu (Industrial Property Act) itakayojumuisha vifungu vya ulinzi na kuweka utaratibu mzuri na rafiki wa kusajili na kulinda Maumbo na Michoro Bunifu nchini.
“Wakati hatua za kukamilishwa kwa sheria hiyo zinaendelea, bado wabunifu wanaweza kulinda bunifu hizo kupitia ARIPO kwa kuchagua Tanzania kama moja ya nchi ubunifu huo unaweza kulindwa,” amesema.
Awali, Nyaisa amesema Tanzania ni moja ya nchi wanachama wa Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO) na Shirika la Miliki Ubunifu la Kanda ya Afrika (ARIPO) baada ya kusaini na kuridhia mikataba na itifaki mbalimbali zinazohusu usimamizi na uratibu wa miliki bunifu kikanda na kimataifa.
Hata hivyo, imeelezwa bado kuna changamoto kwa baadhi ya watu wanaofanya bunifu kutokuwa na mwamko wa kuona umuhimu wa kupatia ulinzi miliki bunifu zao.
“Baadhi yao huanza kuhangaika kuzisajili pale wanapoona mtu mwingine ameiga ubunifu huo, elimu inatakiwa kuendelea kutolewa ili wabunifu waone umuhimu wa kusajili bunifu zao,” amesema Dk Perfect Melkiori, mwalimu wa sheria na meneja miliki bunifu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Pia amesema baadhi ya wanafunzi wanapofanya bunifu zao kuanza kuzionyesha hadharani kabla ya kuzipatia ulinzi kwa kuzisajili.
“Changamoto nyingine ipo katika usajili wa hataza, haswa katika upande wa uandaaji wa nyaraka ambapo humlazimu mbunifu anayetaka kusajili kupata mtaalamu atakayemsaidia kuiandaa,” amesema.