Hamas na Israel zinapaswa kuafikiana kusitisha vita Gaza – DW – 06.09.2024

Blinken amesema kile alichokiona ni kwamba asilimia 90 ya masharti yamekubalika, lakini kuna masuala madogo muhimu yanayopaswa kushughulikiwa, kama uwepo wa wanajeshi wa Israel katika eneo la kimkakati la Philadelphi lililoko kusini mwa Ukanda wa Gaza na linalopakana na Misri.

Blinken amesema pia kwamba kuna mianya iliyoachwa wazi katika mpango huo wa amani juu ya ubadilishanaji wa wafungwa wa Kipalestina na mateka wanaoshikiliwa na Hamas.

Netanyahu aishutumu Marekani kwa kuzuia msaada wa silaha

“Natumai katika siku kadhaa sijazo, tutatoa fikra zetu kwa Israel na Qatar na Misri nao wataweza kupeleka ujumbe huo kwa Hamas juu ya namna masuala tata yanavyoweza kujibiwa. Na kisha utakuwa wakati wa pande zote mbili kusema ndio au hapana. Na tutaona itakavyokuwa,” alisema Blinken.

Mwezi Mei mwaka huu Rais Joe Biden  wa Marekani alitangaza mpango wa hatua tatu wa kusitisha mapigano, lakini tangu wakati huo kumekuwa na mianya ya kuziba ili kufikia makubaliano kamili pamoja na kuachiliwa mateka wa Israel.

Kundi la Hamas linapinga uwepo wa vikosi hivyo vya Israel katika eneo la Philadelphi huku Israel kupitia Waziri wake Mkuu Benjamin Netanyahu ikikataa kuliachia eneo hilo.

Baerbock asema msaada zaidi wahitajika Gaza

Israel Tel Aviv | Baerbock na Katz
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akiwa na mwenzake wa Israel, Israel Katz mjini Tel AvivPicha: GIL COHEN-MAGEN/AFP

Kwengineko, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock yuko Israel leo baada ya kutokea Saudi Arabia na Jordan katika juhudi za kushinikiza kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza, pamoja na kuongeza usaidizi wa kibinaadamu katika eneo hilo linalokumbwa na vita.

Baerbock amekutana na mwenzake wa Israel, Israel Katz, mjini Tel Aviv na baadaye amepangiwa kuzungumza na Waziri wa Ulinzi, Yoav Gallant, lakini hakupanga kukutana na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Jeshi la Israel lasonga mbele maeneo ya kati na kusini mwa Gaza

Mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani pia ataelekea katika eneo linalokaliwa kimabavu la Ukingo wa Magharibi atakakokutana na Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestina, Mohammed Mustafa, mjini Ramallah. Baerbock amesema anaamini mamlaka hiyo inaweza kuwa na jukumu kubwa katika utawala wa baada ya vita Gaza.

Huku hayo yakiarifiwa, msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric, amesema hali ya kibinaadamu imezidi kuwa mbaya, ambapo zaidi ya watu milioni moja hawakupata chakula mwezi Agosti katika eneo la kati na kusini mwa Gaza. Amesema licha ya changamoto wanazokumbana nazo, bado shirika hilo na mashirika mengine ya misaada yanafanya kila yawezalo kutoa msaada wa dharura kwa Wapalestina.

Mkutano wa dharura wazungumzia mzozo wa kiutu Gaza

Tangu uvamizi wa wanamgambo wa Kipalestina kusini mwa Israel kusababisha vifo vya takribani watu 1,200 mnamo Oktoba 7, mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya Gaza yamesababisha mauaji ya zaidi watu 40,000.

afp/ap/reuters

Related Posts