Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amefanya mazungumzo na viongozi wa kampuni ya madini ya BHP, inayotarajia kushirikiana na Lifezone Metal kuwekeza katika mradi wa uchimbaji madini ya Nickel, Wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera.
Mradi wa Kabanga Nickel, unaosimamiwa na Tembo Nickel, unatarajiwa kugharimu Dola Bilioni 2.2 za Marekani. Kati ya hizo, Dola Bilioni 1.6 zitatumika kwa ujenzi wa mgodi na shughuli za uchenjuaji wilayani Ngara, na Dola Milioni 600 kwa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha madini (Multi Metals Refinery Facility) katika eneo la Buzwagi, Kahama.
BHP ni moja ya kampuni kubwa tatu za madini duniani, yenye mapato ya Dola Bilioni 60 kwa mwaka. Kampuni hiyo, ambayo ilisitisha shughuli zake barani Afrika miaka 15 iliyopita, sasa imeamua kurejea Afrika kupitia Tanzania.
Waziri Mavunde amewahakikishia wawekezaji kuwa Serikali ya Tanzania inajitahidi kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kufuata falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan. Pia alitembelea teknolojia ya kisasa ya Hydrometallurgy inayotarajiwa kutumika kwenye kiwanda cha usafishaji madini kinachomilikiwa na Tembo Nickel.
#KonceptTvUpdates