Kocha Liogope katabiriwa makubwa huko

KOCHA wa Mtibwa Sugar, Melis Medo amemtabiria makubwa rafiki yake, Kassim Liogope ambaye anaongoza benchi la ufundi kwa muda la Azam FC wakati mchakato wa matajiri hao kushusha mrithi wa Youssouph Dabo ukiendelea.

Liogope ni kocha mpya wa vijana wa Azam FC baada ya kuondoka kwa Mohammed Badru. Msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara 2023/24 alikuwa msaidizi wa Medo kwenye kikosi cha Dodoma Jiji.

Kutokana na kufahamu uwezo wake, Medo amemwelezea Liogope anaweza kuwa mmoja wa makocha wakubwa wa Kitanzania  miaka michache ijayo.

“Haya nayoyasema siyo kwa sababu ya kujiunga kwake na Azam, najua uwezo wake maana nimefanya naye kazi ni mwepesi wa kuusoma mchezo na kujua mbinu gani nzuri kulingana na wapinzani wanavyocheza,” alisema.

“Nimempongeza kwa nafasi aliyopata. Ni wakati wake wa kuendeleza vipaji vya vijana na kwa bahati nzuri hilo (vijana) ni eneo ambalo analifahamu vizuri.”

Kabla ya kula shavu la kuwa msaidizi wa Medo, Liogope alikuwa akifanya kazi kwenye kituo cha JK Park, Dar es Salaam ambako alikuwa akivumbua na kuendeleza vipaji vya vijana wa Kitanzania.

Septemba 3, Azam ilipotoa taarifa ya kuachana na Dabo, ilieleza timu itakuwa chini ya makocha wa vijana akiwemo Liogope ambao  walianza kusimamia programu za mazoezi ambapo mchezo ujao wa ligi itacheza na Simba.

Alipotafutwa kuzungumzia programu za mazoezi zinavyoendelea kipindi hiki cha wiki ya kimataifa, Liogope alisema huu siyo wakati sahihi kuzungumza.

Related Posts