Wasomi wa vyuo wapewa mbinu kujipima

Iringa.  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu, Profesa Joseph Ndunguru, amesema eneo la kwanza la muhitimu wa chuo kikuu analopaswa kujipima ni kutengeneza kitu  kitakachokuwa  suluhisho la changamoto kwenye jamii yake.

Amesema swali hilo litawafanya wang’amue kama elimu waliyohitimu ina manufaa kwa jamii inayohitaji majibu ya maswali yao kutoka kwa wasomi.

Profesa Ndunguru amesema hayo leo Alhamisi Aprili 18, 2024 alipokuwa akizungumza  wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Utafiti ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE).

Amesema utafiti na ubunifu ni eneo muhimu ambalo wasomi lazima wawekeze kwa sababu  jamii ina changamoto nyingi zinazohitaji majibu ambayo yamejificha kwenye tafiti na bunifu.

“Bila tafiti na ubunifu hakuna maendeleo, fanyeni tafiti zenye lengo la kuikomboa jamii na hata huu uchumi wa viwanda unao zungumzwa unahitaji tafiti na ubunifu,” amesema Profesa Ndunguru.

Amesema ili Tanzania izalishe bidhaa zitakazoshindana kwenye soko la kimataifa, lazima vyuo vikuu vilivyopo viwekeze kwenye tafiti na ubunifu.

“Hata kwenye kilimo, ili ufanye mageuzi kwenye kilimo unahitaji tafiti na ubunifu. Tafiti na bunifi zitaongeza tija, bei za vyakula zitapungua na usalama wa chakula utaongezeka,” amesisitiza Profesa Ndunguru.

Hata hivyo, ameahidi kutoa ufadhili wa kufanya tafiti kwa wanafunzi watano wanaosoma ngazi ya shahada ya pili.

Awali, baadhi ya wasomi wa MUCE wamesema mbali na ubunifu, tafiti zinahitaji fedha jambo ambalo wanapambana nalo.

Mhadhiri wa MUCE, Dk Philpo John amesema wanaendelea kufanya tafiti mbalimbali kwa ubunifu ili kusaidia jamii inayo wazungika.

Zaidi ya tafiti 66 zinawasilishwa kwenye maonyesho nyingi zikiwa na ubunifu.

Related Posts