Mfanyabiashara kortini akidaiwa kujipatia Sh438 milioni kwa udanganyifu

Shinyanga. Mfanyabiashara na mkazi wa Ilala jijini Dar es Salaam, Sharifa Ibrahim (32) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Mfanyabiashara huyo anayedaiwa kutenda makosa hayo akiwa na wenzake (idadi haijatajwa), amefikishwa na kusomewa mashtaka matatu katika kesi ya uhujumu uchumi namba 000024322/2024, mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Mwakihaba Gabriel.

Akimsomea mashtaka hayo, Mwendesha Mashtaka Louis Boniface amesema shtaka la kwanza ni kuongoza genge la uhalifu kinyume na kifungu namba 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi namba 200 marejeo ya mwaka 2022.

Shtaka lingine ni kujipatia Sh428.7 milioni kwa njia za udanganyifu kinyume na kifungu namba 302 cha Sheria ya Makosa ya Jinai, sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

Alisema mshtakiwa (Sharifa) kwa makusudi na kujua kupitia Kampuni ya Tanzlobal Company Limited alitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Januari hadi Mei 27, 2023,” amesema Boniface.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka (Boniface), shtaka la tatu linamkabili mwanamke huyo ni kutoa hundi isiyokuwa na fedha za malipo benki kinyume na kifungu namba 332B (1), (3) na (4) cha Kanuni ya Adhabu namba 16 marejeo ya mwaka 2022.

Mshtakiwa ambaye anawakilishwa na Wakili Erick Mutta na Allan Robi, baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili, hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza shauri hilo.

Mwendesha Mashtaka ameiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa, huku mshtakiwa akienda rumande kutokana na mashtaka hayo kutokuwa na dhamana.

Hakimu Mwakihaba ameahirisha shauri hilo hadi Jumatatu Septemba 9, 2024 litakapoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Related Posts