Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana ametoa wito kwa wananchi kupanda mazao yasiyowavutia tembo, kama ufuta, ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na wanyamapori hao.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 6, 2024, wakati wa kikao na baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, kilichofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni jijini Dodoma.
Dk Chana amesema Serikali inachukua hatua mbalimbali kuwalinda wananchi dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu, ikiwemo kutumia teknolojia ya kuwavalisha tembo kola maalumu, ambazo zinasaidia kufuatilia mwenendo wa makundi ya tembo na kuelewa wapi wanaelekea.
Pia, Serikali inaendelea kujenga vituo vya askari wanyamapori katika maeneo yanayoathiriwa zaidi na tembo ili kutoa ulinzi wa haraka.
Mbali na hayo, Dk Chana amesisitiza kuwa Serikali imeagiza kuwekwa vibao vya tahadhari katika maeneo ambayo ni njia za kawaida za wanyamapori ili kuwatahadharisha wananchi kuepuka kupita huko kwa usalama wao.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Meatu, Leah Komanya, ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jitihada zake katika uhifadhi na kupambana na changamoto ya wanyamapori wakali, hasa tembo.
Amesema wizara imeisaidia Wilaya ya Meatu kwa kutoa gari, pikipiki nne na kujenga kituo cha askari wanyamapori ili kukabiliana na wanyama waharibifu.
Awali, Diwani wa Kata ya Mwandoya, Basu Kayungilo, amewasilisha taarifa ya Baraza la Madiwani kuhusu athari zinazowakumba wananchi wa vijiji vilivyoko karibu na Pori la Akiba la Maswa na Jumuiya ya Wanyamapori ya Makao, akisisitiza umuhimu wa kufikiwa kwa muafaka kuhusu malipo ya kifuta machozi kwa waathirika wa wanyamapori pamoja na mgawanyo wa asilimia 25 ya mapato yanayotolewa kwa vijiji jirani na hifadhi hizo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na watumishi waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wanaohusika na masuala ya wanyamapori, ambapo walijadili mikakati zaidi ya kuhakikisha usalama wa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya wanyamapori.