Hanang. Wakazi wa Kijiji cha Gocho kilichopo Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, wamekumbwa na taharuki baada ya Mlima Hanang kumeguka na kusababisha mafuriko na kuharibu mazao na makazi ya watu.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 30, 2024, wamesema tukio hilo limetokea jana Aprili 29, 2024 usiku kwenye kijiji hicho.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Aloyce Hams amesema wakiwa wamelala walishtushwa na kelele za maji ya mafuriko yaliyokuwa yanatokea Mlima Hanang’.
“Tunamshukuru Mungu hakuna vifo wala majeruhi lakini baadhi ya mazao yetu yamesombwa na maji na nyumba mbili zimebomoka,” amesema.
Amesema hii ni mara ya kwanza kwenye maisha yake ya miaka 35 aliyoishi kijiji cha Gocho kuona mafuriko makubwa kama hayo.
Mkazi mwingine, James Hotay amesema wanamshukuru Mungu hakukutokea vifo wala majeruhi kwenye mafuriko hayo.
“Hii ni tofauti na tukio la mwaka jana la Mlima Hanang kule Gendabi kwani mafuriko haya yalikuja usiku yakiwa na maji mengi na siyo tope, magogo na majabali makubwa,” amesema Hotay.
Ameiomba Serikali kuwapatia maeneo mengine ya kuishi ili kuondokana na hofu na taharuki ya kukaa kwenye eneo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Almishi Hazali amewataka wakazi wa eneo hilo kutokuwa na hofu kwani wataalamu na viongozi wamefika eneo hilo kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo na kufanya tathmini.
“Jamii ikae kwenye hali ya utulivu na kutoa ushirikiano kwa wataalamu watakaokuja kwenye kijiji chenu hata kamati ya usalama inakuja, kusiwe na ushabiki ila uhalisia,” amesema.
Amewataka wakazi hao wawe na tahadhari, maji yakiongezeka ili kusitokee madhara zaidi yatakayosababishwa na mafuriko hayo.
Disemba 3, 2023 kwenye Mlima Hanang, kulitokea maporomoko ya tope, mawe na magogo na kusababisha vifo vya watu 89, majeruhi na kuharibu makazi na mashamba ya watu. Serikali ilirekebisha miundombinu na kutoa msaada kwa waathirika wa mafuriko hayo.