KAIMU Kocha Mkuu wa Simba SC, Juma Mgunda, ameanza majukumu yake ndani ya kikosi hicho kwa kuambulia sare katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo FC.
Mchezo huo uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa mkoani Lindi, umemalizika kwa sare ya mabao 2-2 ikiwa ni sare ya tatu mfululizo kwa timu hizo zilipokutana katika mechi za karibuni.
Mgunda ambaye amekabidhiwa kikosi hicho hivi karibuni baada ya Simba kuachana na Kocha Mualgeria, Abdelhak Benchikha, ilianza kufunga bao dakika ya 34 kupitia Willy Onana aliyepokea pasi ya Mohamed Hussein.
Dakika tano baada ya Simba kuwa mbele, Kelvin Sabato alisawazishia Namungo, akifunga bao lake la kwanza msimu huu ndani ya ligi hiyo.
Kuingia kwa bao hilo ambalo Sabato alifunga kupitia pasi ya Ayoub Semtawa, liliifanya Simba kuamka tena, lakini juhudi zao hazikuzaa matunda wakajikuta dakika 45 za kwanza matokeo kuwa sare ya bao 1-1.
Katika kipindi hicho cha kwanza, Kiungo Mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis alishindwa kuendelea na mchezo kutokana na rafu aliyochezewa na Hamis Halifa dakika ya 25, akatolewa dakika ya 27 na nafasi yake ikachukuliwa na Pa Omar Jobe.
Mapema tu kipindi cha pili, Mgunda alifanya mabadiliko ya kumtoa Babacar Sarr, nafasi yake ikachukuliwa na Hamis Abdallah ambaye kwa kiasi fulani alienda kupambana kuhakikisha timu inakuwa imara eneo la kiungo.
Kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo huo hadi kufikia 61, ilishuhudiwa Simba ikipiga kona tano huku Namungo ikiwa haijafanikiwa. Licha ya Simba kupiga kona nyingi, lakini walishindwa kuzitumia vizuri.
Katika kuhakikisha kila upande unasaka ushindi baada ya muda mrefu matokeo kuwa sare ya bao 1-1, mabadiliko kadhaa yalifanywa ambapo dakika ya 67 Kocha wa Namungo, Mwinyi Zahera, aliwaingiza Hassan Kabunda na Meddie Kagere kuchukua nafasi ya Semtawa na Sabato.
Muda mfupi baada ya kuingia kwa wachezaji hao, Simba wakaongeza bao la pili dakika ya 69 kwa mpira wa adhabuya moja kwa moja iliyopigwa na Edwin Balua, ambaye alimtesa kipa wa Namungo, Jonathan Nahimana. Balua katika mchezo huo, ilikuwa ni mara yake ya kwanza anaanza kikosi cha kwanza ndani ya Simba aliyojiunga nayo kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea Tanzania Prisons.
Zahera akaendelea kupambana kuhakikisha hawapotezi nyumbani, akafanya mabadiliko mengine dakika ya 78 akiwatoa Frank Domayo na Hamis Halifa, wakaingia Hashima Manyanya na James Mwashinga.
Mabadiliko hayo kwa kiasi kikubwa yalichangia Namungo kuongeza nguvu za mashambulizi ambapo dakika ya 89, wachezaji wa timu hiyo waligongeana pasi za harakaharaka kabla ya Kagere kuwachonganisha kipa wa Simba, Ayoub Lakred na beki wake Kennedy Juma na hivyo akajifunga na kufanya ubao wa matokeo kusomeka 2-2.
Sare hiyo inaifanya Simba kufikisha pointi 47 baada ya kucheza mechi 22 na kusalia nafasi ya tatu katika msimamo, huku Namungo iliyocheza mechi 24 ikiwa nafasi ya tisa kwa kukusanya pointi 27.
Mabao mawili waliyoruhusu Simba katika mchezo huo, yameifanya timu hiyo kuendelea kuwa na rekodi mbovu ya safu yao ya ulinzi ikifungwa mabao 23 katika mechi 22.