KAMA wewe ni beki wa kati unaitumikia klabu nyingine iwe ndani au nje ya nchi, kisha ukifuatwa na yeyote na akakuambia kwamba Yanga inataka kukusajili usimuamini sana mtu huyo, kwani huenda ni matapeli.
Si huwa mnaona tangazo linaloandikwa katika kuta za nyumba ambayo haiuzwi likitanguliwa na onyo lisemalo; ‘Ogopa Matapeli….NYUMBA HII HAIUZWI’.
Basi hivyo ndivyo ilivyo nafasi ya beki wa kati ya Yanga kutokana na viwango bora na umahiri wanaouonyesha mabeki watatu wazawa Dickson Job, Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto ambao katika ligi wamefunika hadi rekodi za wababe wa Afrika Al Ahly na Mamelodi Sundowns.
Mabeki hao wa kati ni kama wamejimilikisha nafasi hiyo kiasi cha kuwakimbiza wageni wanaosajiliwa, lakini hata katika timu ya taifa ‘Taifa Stars’ jamaa wana hatimiliki. Ndiyo maana hata mabosi wa Yanga huwa wanahangaika kufanya usajili katika maeneo mengine ikiwamo beki za pembeni, kiungo na ushambuliaji, lakini husikii wanapata presha kwa beki ya kati kwa sababu ya kazi zinazofanywa na kina Bacca.
Eneo la beki wa kati siyo kwamba halifanyiwi maboresho kunasa saini ya mabeki wa kigeni hufanya hivyo, lakini mambo yanakuwa magumu kwa wageni kutoboa mbele ya kina Bacca.
Kama hujui tu katika nafasi zote uwanjani, kuna moja ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitawaliwa na wazawa na usajili utakavyofanyika, ataingia mgeni mtihani kwake ni namna anavyopambania kuwang’oa.
Utatu huo umekuwa imara kwa misimu mitatu mfululizo ambapo mbali na kukiwasha kwa mafanikio, lakini umekuwa pia ni tegemeo Taifa Stars. Rekodi zinaonyesha katika misimu mitatu Yanga iliruhusu jumla ya mabao 40 tu katika mechi 90 za Ligi Kuu, kwani 2021-22 ilifungwa manane, 2022-2023 iliruhusu 18 na msimu uliopita ilifungwa 14 ikiwa timu iliyoruhusu mabao machache mno.
MAMELODI, AL AHLY WANASUBIRI
Rekodi za ulinzi za mabeki wa Yanga, zimezipiku rekodi za wababe wa soka la Afrika, Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ukijumlisha matokeo ya timu hizo kwa misimu mitatu iliyopita kuanzia 2021/22, 2022/23 na 2023/24.
Katika misimu mitatu mfululizo iliyopita ambayo Mamelodi Sundowns imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), imeruhusu jumla ya mabao 44, ambapo msimu wa 2021/22 iliruhusu mabao 20, msimu wa 2022/23 (mabao 13) na msimu uliopita wa 2023/24 (mabao 11).
Kwa upande wa Al Ahly ya Misri, katika misimu mitatu iliyopita ambayo miwili imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na mmoja kumaliza katika nafasi ya tatu, imeruhusu jumla ya mabao 62, ambapo msimu wa 2021/22 iliruhusu mabao 21, msimu wa 2022/23 (mabao 13) na msimu uliopita wa 2023/24 (mabao 28) japo ligi ya Misri kila timu inacheza mechi 34 tofauti na Tanzania na Afrika Kusini ambazo kila timu hucheza mechi 30.
Tangu Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alipotua na kujenga ufalme Yanga akitokea Malindi ya Zanzibar, klabu hiyo imepita mabeki wa kati wengi wazawa wakiwemo Kelvin Yondani, Hamis Yusuf, Lulanga Mapunda, George Owino (Kenya), Shaibu Abdallah ‘Ninja’. Ubora ulioanzishwa na Cannavaro na Yondani kwa miaka ya hivi karibuni umeifanya timu hiyo kuwa na mwendelezo wa kusajili mabeki wa kati wazawa ambao wamekuwa chachu hadi timu ya taifa.
Hivi sasa wanatamba kina Mwamnyeto na miaka ya nyuma ilikuwa hivyo kwa kina Cannavaro kuanzia Yanga hadi Taifa Stars.
Uwepo wa mastaa wazawa umepangua mastaa kadhaa wa kigeni waliopewa mkono wa kwaheri kutokana na kushindwa kuonyesha ushindani mbele ya kina Bacca wakiwamo Gift Fred, Mamadou Doumbia na Lamine Moro aliyecheza kwa kiasi tofauti na wengine.
Makocha kadhaa walioifundisha Yanga wamekuwa wakiwatumia wachezaji hao kwa kupokeza nafasi na wakati mwingine kuanzishwa wote ili kutengeneza ubuta imara ulioiwezesha kwa misimu mitatu mfululizo kutawala soka la Tanzania ikibeba ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.
Pia ni wachezaji haohao wakishirikiana na wengine wa nafasi zilizosalia waliofikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na msimu uliopita kuandika historia ya kutinga makundi ikiishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ikiwa ni baada ya kupita miaka 25 tangu Yanga ilipofanya hivyo 1998.
Mwanaspoti limezungumza na makocha na wachezaji waliofunguka faida ya Yanga kutotumia wageni kwenye nafasi hiyo.
Ujio wa Mwamnyeto, Job na Bacca wamepishana na mabeki bora wazawa waliokuwa Yanga yaani pacha ya Yondan na Cannavaro’ waliocheza kwa mafanikio makubwa na hata Taifa Stars.
Yondani ambaye kwa sasa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Geita Gold aliliambia Mwanaspoti kuwa wazawa ndani ya Yanga ni mwendelezo wa ubora wa nyota waliowatangulia ambao hawakufanya makosa.
“Nashukuru nilipata nafasi ya kuitumikia timu hiyo, siwezi kujisifu nilikuwa bora wadau wa mpira walishuhudia tulichokifanya na uwepo wa kina Mwamnyeto, Bacca na Job ni mwendelezo wa matunda yetu,” alisema Yondani aliyetua Yanga 2012 akitokea Simba.
“Tusingefanya kilicho bora uongozi ungekosa imani na wazawa, lakini kwa kuwa tulithubutu ndiyo maana hili linaendelea na nawapongeza waliopo wanafuata njia sahihi wanapambana na kufanya mambo makubwa.”
Yondani alisema ubora wa ukuta Yanga unajenga imani na kutengeneza kizazi ambacho kitakuja kucheza eneo hilo ambalo tayari limewekwa kwa ajili yao.
“Hakuna beki mzawa anayehitajiwa na Yanga anayecheza nafasi ya kati atakuwa anasita kujiunga na timu hiyo kwani ana uhakika wa kucheza tofauti na Simba yenye mchanganyiko wa wageni na wazawa,” alisema.
Kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alisema Yanga imemrahisishia kupata mabeki wenye muunganiko wa muda mrefu. “Hakuna eneo gumu na linaloumiza kichwa kama eneo la ulinzi hasa mabeki wa kati. Ndiyo safu ambayo haifanyiwi mabadiliko mara kwa mara tofauti na nafasi nyingine,” alisema.
“Muunganiko walionao Yanga siyo sababu ya kuwajumuisha Stars, bali wamekuwa wakifanya vizuri na ndiyo sababu ambayo imekuwa ikilishawishi benchi la ufundi kuwajumuisha kikosi cha Stars.
“Siyo tu kwa Stars, lakini ukuta huo ni darasa kwa wachezaji wengine wanaocheza nafasi hiyo kujifunza vitu kutoka kwa Mwamnyeto, Bacca na Job ambao wamekuwa na mafanikio makubwa.”
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi akizungumzia ubora wa mabeki hao alisema licha ya kuwakuta anafurahishwa na namna walivyopigania kulinda ubora.
Alisema mabeki hao watatu wamekuwa mhimili mzuri wa kikosi wanaompa machaguo ya nani aanze, huku wengine wakiwa na uwezo wa kutumika nafasi tofauti na walizozoeleka.
“Nilipofika hapa nilikuta sehemu kubwa ya safu ya ulinzi ipo sawa. Tulikuwa na kazi ya kuongeza watu wawili au mmoja tu, ilikuwa hatua nzuri kwetu kuwakuta mabeki wa kati wapo imara na wenye rekodi ya kazi nzuri,” alisema Gamondi.
“Kwa viwango vyao hatukuwa na sababu tena ya kuanza kufikiria watu wapya kwa kuwa hawa waliopo wanafanya vizuri, unaweza leo umtumie huyu au ubadilishe vingine. Kitu kizuri hapa zaidi ni kwamba mabeki wote watatu ni Watanzania na wanafanya vizuri hadi timu ya Taifa.”
Gamondi aliongeza: “Kuna mabeki wameondoka, lakini siyo kwamba ni wabovu, kitu kizuri kwa mchezaji ni kupata muda wa kucheza. Ndiyo maana mliona beki kama Gift (Fred) alikuwa mchezaji mzuri sana, ila hakupatiwa muda kiasi wa kucheza ili asipoteze kipaji chake. Hawa mabeki mfano Job anaweza kutumika pembeni angalia Mwamnyeto kuna wakati tulikuwa tunampa nafasi ya kucheza kama kiungo mkabaji. Hizi ni baadhi ya faida kwa Yanga na Tanzania.”