Waganga wetu kumbe nao wamerogwa

Amini usiamini katika miaka ya nyuma watu waliokuja kujitafuta mjini waliogopa kurudi vijijini walikozaliwa. Kulikuwa na kitisho cha imani za ushirikina hivyo waliogopa kurogwa. Waliomudu kwenda huko walihakikisha wanabeba magunia ya sukari kwa ajili ya kugawa kwa wanakijiji. 

Waliogopa kuonekana wanaringia mafanikio yao, na kwamba wangerudishwa kwenye statasi za wenyeji hata kwa kutiwa uchizi.

Hali hii ilisababisha maendeleo kuchelewa kufika vijijini. Wakati mwingine changamoto za ukosefu wa maji salama na miundombinu ya kijiji hazikupaswa kutupiwa Serikali kuu. 

Kuna wataalamu wengi waliotokea hapo kijijini wangeweza kuzitatua. Walimu na mainjinia waliopata elimu ya juu na kuishi mjini wangeweza kusaidia maendeleo ya vijiji vyao. Lakini waliogopa kuzimwa data kwani wachawi hawana sera ya “elimu ya kizungu” zaidi ya kurithishana tunguli.

Mtu yeyote mwenye ndoto za mafanikio anakosa amani anapofikiria kuzimwa kwa ndoto zake kirahisi. Pamoja na kuambiwa kuwa sumu ya uchawi ni uganga, watoto wa mjini wanaogopa kusikia “mchawi wako kafa”.

 Usemi huu unamaanisha mchawi aliyekuroga ambaye ndiye pekee anayejua ufumbuzi wa tatizo lako, anakufa na siri hizo. Ina maana utaendelea kupigika maana hatokuwepo mwingine mwenye dawa yako.

Au unaambiwa “mganga wako karogwa”. Wakati nyote mnaamini kuwa mganga fulani ndiye kiboko ya wachawi, anatokea bingwa anayemroga mganga huyo. Sijui mtakuwa na hali gani mnapoona mtandao mzima wa waganga unashindwa kumwokoa mshirika wao. Pengine mtakuwa sawa na Wafilisti waliomwamini Goliati kuwa ndiye mwamba wa dunia, lakini akadondoshwa na kijana mdogo mchunga kondoo. 

Hivi sasa mijini ndiyo kwenye imani za ushirikina zaidi ya vijijini. Mpaka leo wengi wanashindwa kuwatofautisha waganga na wachawi. Mara nyingi watu huenda kwa wachawi kudidimiza maendeleo, kukomoa au kulipa kisasi katika mambo yanayowakwaza wakidhani wanaenda kwa mganga.

Pengine mwanandoa anamwajiri mtaalamu wa kumzevenza mwenzi wake kwa limbwata, na akamchukulia mtaalamu huyo kuwa mganga wake.

Mganga na mchawi wanatofautiana sana kwenye kazi zao. Imenenwa kuwa tutautofautisha mti kutokana na matunda yake. Mche wa karanga unafanana na ule wa mbigiri, lakini matunda yake yanatofautiana sana. Ni kama vile mlimao unavyofanana na mchungwa. Mwisho wa siku matunda yake yanajitanabaisha. 

Kwa tafsiri yangu na mchawi ni mlozi. Yeye anahusika kwenye mateso, uharibifu na maangamizi. Na mganga ni tabibu au muuguzi mwenye jukumu la kupambana na wachawi na kazi zao. Hawa wawili wanakutana kwenye mapambano mmoja akitega na mwingine akitegua. Wanatuchanganya kwa vile mganga anavyojua mitego ya kichawi, maana huwezi kuutegua mtego usioweza kuusuka. 

Kazi hizi mbili zina masharti na miiko inayoshabihiana kwa kiasi. Mwiko mkuu ni kutokutoa siri. Uchawi ni sawa na mtandao wa kigaidi, ndiyo maana kazi zao hufanywa gizani. Siri zake haziwekwi hadharani hata kwa mlungula au mateso. Wenyewe wapo tayari kumuua yeyote atakayekusudia kuwataja wenzake. Waganga nao wana siri kubwa inasemekana kwa kulinda kazi hiyo isiingiliwe na mumiani. 

Inasemekana waganga wa kweli hawapo kibiashara, bali hujitolea na kupokea sadaka ya mizimu kama malipo baada ya kazi ngumu ya kuokoa maisha. Ndio maana wanaishi kwenye vijumba dhaifu na hawana mbwembwe za kimaisha. Hujivika mavazi duni na kula chakula rahisi. Hapa nazungumzia waganga wa enzi hizo, siyo hawa wa leo wa fedha za majini na mawakala wa freemason. 

Wakati huu tulionao unatisha maradufu. Waganga wameshindwa masharti na sasa wameingia kwenye biashara. Wameshindwa masharti na vipawa vyao kuondoka. Sasa huwezi kujua yupi ni yupi kwani hakuna tena mteja anayewafuata kwa shida za tiba, shida ni fedha na utajiri. 

Ushirikina umekamata kwenye sekta zote muhimu kuanzia ofisi za Serikali hadi nyumba za ibada. Yaani ukipigwa huna pa kukimbilia; ukirogwa mtaani ukakimbilia kwa mganga, unapigwa tena. Ukikimbilia nyumba za ibada unakutana na yaleyale. Yaani ni sawa unamkimbilia jambazi baada ya kumkwepa kibaka! Tangu lini mganga akamtuma mgonjwa amletee viungo vya binadamu?

Habari nyepesi zinanong’ona kuwa matukio ya uhalifu wa kimazingara yanashamiri kwenye mikusanyiko na nyakati za matukio makubwa. Kwa mfano hivi sasa tukielekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, wimbi hili limekuwa kubwa zaidi. Hata kama wanasiasa nao wamo, lakini ni lazima wahalifu watatembelea nyota zao. Hii ndiyo sababu kila kukicha tunakutana na matukio ya watu kutekwa, kupotea na kuuawa kwenye mazingira tatanishi.  

Athari zinazoachwa na wahalifu wa kimazingara ni kubwa sana. Utaona katika hali ya kawaida, mtu anapoua hubaki na wenge.
 Ataendelea kuua maisha yake yote. Hivyo tutegemee ongezeko la vitendo hivyo harami kadiri siku zinavyokwenda.

Baada ya sheria ya uhalifu wa kimtandao kuonesha mafanikio makubwa, naishauri Serikali yetu sikivu kutunga sheria ya uhalifu wa kimazingara. Potelea mbali wasiamini uchawi, lakini mtu yeyote atakayekutwa na hatia za ramli chonganishi au ushirikina ashughulikiwe kivingine.
 

Related Posts