Mtoto Mchanga anayekadiriwa kuwa na umri wa siku kadhaa amekutwa ametupwa kwenye shimo la choo katika mtaa wa Idundilanga halmashauri ya mji wa Njombe huku mama yake akiwa bado hajatambulika.
Fioteus Ngilangwa ni mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo ameieleza Ayo TV kuwa alipokea taarifa ya uwepo wa mtoto huyo ndani ya shimo kwenye nyumba ambayo hakuna mtu anayeishi na kufika kwa ajili ya uokoaji huku pia wakitoa taarifa kwa jeshi la Polisi.
“Mtoto tumekuta ameshafariki kwasababu aliyemtupa alikuwa ameshatenganisha mtoto na kondo peke yake na kwa taarifa nilizonazo makazi haya hakuna mtu anayeishi kwasababu hii nyumba kuna mtu alinunua lakini haishi hapa”amesema Ngilangwa
Mkaguzi wa jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Njombe Bahati Adamu Mtane amesema wamefika muda mfupi kwenye eneo hilo la Lutilage ili kusaidia uokoaji baada ya kupata taarifa na kumtoa ili mambo mengine yaweze kuendelea huku pia akibainisha kuwa wakati zoezi hilo likiendelea kuna taarifa za kutupwa kichanga kingine kwenye eneo jingine ambako pia jeshi la Polisi limeelekea kwa ufuatiliaji zaidi.
“Inawezekana kichanga hiki kimetupwa ndani ya siku tatu hizi na ni mtoto wa kike lakini nitoe wito kwa jamii kuacha vitendo hivi maana yake kama alitupwa akiwa hai basi amekatishwa uhai wake na hivi tunavyoongea kuna eneo lingine kichanga kimetupwa na wenzetu wameenda kuchukua kichanga hicho”amesema Mtane
The post Vichanga watupwa chooni Njombe,Polisi watoa onyo first appeared on Millard Ayo.