Aga Khan kuchunguza maumivu ya mgongo bure

Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan kesho Jumapili, inatarajia kufanya uchunguzi wa maumivu ya mgongo bure na mpango matibabu kwa punguzo la hadi asilimia 50, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Fiziotherapia (tiba mazoezi).

Aga Khan inafanya hivyo kuungana na mataifa mengine katika kuadhimisha siku hiyo  inayoadhimishwa kila mwaka siku ya Septemba 8.

Taarifa iliyotolewa jana Septemba 7, 2024 na Mratibu wa habari wa Taasisi ya Huduma za Afya za Aga Khan, Tanzania, Geofrey Anael imeeleza kuwa wagonjwa watakaofika kesho watapewa vipimo na uchunguzi bila malipo.

“Dhima ya mwaka huu inalenga kutatua tatizo la maumivu ya mgongo (LBP), tatizo linalosumbua mamilioni ya watu duniani, Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam imejizatiti kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa fiziotherapia katika kuimarisha afya pamoja na  mijongeo ya mwili na viungo,” amesema.

Anael amesema katika kutambua siku hii muhimu, Hospitali ya Aga Khan imefanya kambi ya uchunguzi wa bure kwa wote wenye maumivu ya mgongo walioweza kushiriki.

Pia, washiriki watanufaika na elimu ya bure kuhusu maumivu ya mgongo na namna ya kuyadhibiti, ushauri wa bure na wafiziotherapia na kupatiwa mpango matibabu kwa punguzo la hadi asilimia 50.

“Kama hospitali pekee yenye hadhi ya kimataifa ya ubora wa huduma za afya (JCIA accreditation) nchini, Hospitali ya Aga Khan inajitolea kutoa huduma maalum za kitaalamu ili kusaidia kuboresha afya katika jamii, kupitia uelimishaji kuhusu mikakati ya kudhibiti maumivu ya mgongo, kuweka mipango maalum ya mazoezi ya viungo, na matibabu ya fiziotherapia.”

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Simion Gundah, Mkuu wa Idara ya Fisiotherapia hospitali ya Aga Khan, amesisitiza umuhimu wa fiziotherapia katika kutibu na kudhibiti maumivu mbalimbali ya viungo.

“Fiziotherapia ni ufunguo wa kuishi bila maumivu ya viungo, ambapo uimara wa migongo yetu unasaidia nguvu za maisha yetu,” amesisitiza jinsi afya ya mgongo ilivyo muhimu kwa ustawi na ubora wa maisha kwa jamii.

Siku ya fiziotherapia Duniani, iliyoanzishwa na Shirikisho la Kimataifa la fiziotherapia mnamo mwaka 1996, inasisitiza jukumu muhimu la fiziotherapia katika kudhibiti na kuzuia maumivu ya chini ya mgongo (LBP).

LBP ni tatizo kubwa la afya duniani, likiwaathiri takribani watu milioni 619 mwaka 2020 na pia ni chanzo kikuu cha ulemavu.

Anael amesema tatizo hilo linaweza kumuathiri mtu yeyote na mara nyingi haliwezi kubainishwa kwa sababu moja inayojulikana.

“Unafuu kupitia fiziotherapia ni muhimu kwa kudhibiti maumivu ya mgongo kwa ufanisi, kwani huimarisha afya kwa ujumla na kupunguza uwezekano wa maumivu ya baadaye,”amesema.

Related Posts