Notisi ya TAA kwa kampuni ya ndege yakwama kwa muda

Arusha. Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Septemba 2, 2024, iLItoa zuio la muda linalozuia notisi inayoitaka Kampuni ya Ndege ya W-Cargo Airline Limited kuondoka katika eneo linalomilikiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Uamuzi huo umetolewa kutokana na maombi ya zuio yaliyowasilishwa mahakamani hapo na kampuni hiyo,  ikiomba Mahakama itoe zuio la muda hadi kesi ya msingi ya ardhi namba 17632/2024 itakapotolewa uamuzi.

Maombi hayo ya zuio la muda kusubiri uamuzi wa kesi ya msingi ambapo kwa mujibu wa kampuni hiyo ya ndege, kuna mgogoro baina ya pande hizo unaotokana na mkataba wa ukodishaji.

Hata hivyo, wakati wakisubiri uamuzi, kampuni hiyo iliwasilisha maombi ya zuio ikiiomba mahakama hiyo iamuru hali iendelee kuwa kama ilivyo kwa sasa hadi maombi ya msingi yatakaposikilizwa.

Jaji Lusungu Hemed, alisikiliza maombi hayo namba 19161/ 2024 ambapo mjibu maombi wa kwanza alikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Jaji Hemed alikubaliana na maombi hayo na kuamuru hali iendelee kuwa kama ilivyo hadi kesi ya ardhi namba 17632/2024 itakapotolewa uamuzi na kila upande kubeba gharama zake.

Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na kampuni hiyo ya ndege chini ya vifungu vya 68(e), 95 na Amri ya XXXVII Kanuni ya 2(1) ya Kanuni ya Mwenendo wa Madai, ikiomba zuio la muda kwa TAA.

Wakili Alex Balomi aliiwakilisha kampuni hiyo mahakamani ambapo aliiomba Mahakama kupitisha hati ya kiapo ili kuunga mkono ombi hilo.

Maombi hayo ya zuio la muda, masharti elekezi ni yale yaliyoainishwa katika kesi ya Atilio dhidi ya Mbowe (1969) HCD 284, katika kesi hiyo mahakama iliweka masharti matatu ya kuzingatiwa na Mahakama kabla ya kukubali au kukataa ombi la zuio.

Masharti hayo ni lazima kuwe na jambo la kimantiki ambapo mdai au muombaji ataweza kushinda, mwombaji atapata hasara isiyoweza kurekebishwa inayohitajika kuingiliwa kati kwa mahakama kabla ya haki ya kisheria ya waombaji kuthibitishwa.

Sharti la tatu likiwa ni kulinganisha au mlinganisho wa kutotoa zuio, mwombaji atapata hasara kubwa kama wataruhusu pabomolewe.

Jaji Hemed amesema imethibitika kuwa kampuni hiyo ya ndege ni mpangaji katika kiwanja kilichopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ndani ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

TAA iliiipa kampuni hiyo ya ndege notisi ya kuondoka katika eneo hilo ambalo kampuni hiyo inapinga na kulingana na kampuni hiyo ya ndege, kuna mgogoro kati ya wahusika unaotokana na mkataba wa ukodishaji.

Kampuni hiyo ya ndege imedai kuwa ilipata milki na hivyo kuboresha kwa kiasi kikubwa eneo lililokodishiwa na kuwa ilikuwa inatimiza makubaliano ya kimkataba na kuwa ikifukuzwa katika eneo hilo, itapata hasara isiyoweza kufidiwa katika biashara.

Jaji huyo amesema kesi ya msingi ipo na imeelezwa katika hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo,  kuwa kuna mgogoro unaotokana na mkataba wa upangaji ambapo kampuni hiyo inadai TAA imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa mkataba.

Amesema anafahamu kampuni hiyo ya ndege imeshafungua kesi ya ardhi.

Kuhusu sharti la pili Jaji amesema kampuni hiyo imeeleza kuwa imewekeza fedha nyingi na ikifukuzwa itapata hasara isiyoweza kurekebishwa kibiashara.

“Nimezingatia ukweli kwamba mwombaji ni kampuni inayojishughulisha na biashara inayohusiana na ndege katika eneo hilo na ikifukuzwa itapoteza sifa yake katika biashara,” amesema jaji na kuongeza.

“Kwa maoni yangu kupoteza sifa hakuwezi kulipwa kupitia njia za fedha,ni maoni yangu kuwa sharti la pili limefikiwa,”

Kuhusu sharti la tatu amesema kampuni hiyo ya ndege ndiyo itakayopata shida kuliko TAA ikiwa zuio la muda halitatolewa,  kwani itafukuzwa katika eneo  na kwa upande wa wajibu maombi ikiwa amri za zuio zitatolewa, bado watakuwa na haki ya kulipwa kodi inayodaiwa (ikiwa ipo).

“Katika uchanganuzi wa mwisho, naona masharti yote katika Atilio dhidi ya Mbowe (supra) yametimizwa kwa jumla. Kwa maana hiyo, ninaendelea kukubali ombi kwamba hali iendelee kuwa kama ilivyo “STATUS QUO”, ikisubiri kuamuliwa kwa kesi ya ardhi namba 17632 ya 2024, kila upande utabeba gharama zake,” amesema Jaji.

Related Posts