CBE Mbeya kuwajengea uwezo wakulima, wafanyabiashara wa parachichi

Mbeya. Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Mbeya, kimepanga kuwajengea uwezo wafanyabishara wa kimataifa, wamiliki na wazalishaji wa zao la parachichi katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini katika kutumia fursa za biashara na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Warsha hiyo itawahusisha wadau kutoka makundi zaidi ya 50 wakiwemo maofisa biashara, ikiwa ni mikakati ya Serikali kuhakikisha wanapatiwa elimu bure ya fursa za uwekezaji na masoko, ili kukuza sekta ya ajira na uchumi endelevu kwa Watanzania.

Mkurugenzi wa Chuo cha CBE, kampasi ya Mbeya, Jeremiah Wilhelm amebainisha hayo leo Jumamosi Septemba 7,2024 wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kuhusu kuanzishwa kwa  mitalaa mipya minne sambamba na ujenzi wa bwalo la chakula lenye thamani ya Sh228 milioni litakalohudumia wanafunzi na watumishi 1,000 kwa siku.

Ametaja miongoni mwa mitalaa iliyoelekezwa na Serikali ni pamoja na shahada ya kwanza ya biashara, usimamizi wa masoko, manunuzi ugavi na uhasibu ambazo hazijawahi kutolewa tangu chuo hicho kianzishwe miaka 10 iliyopita.

“Uanzishwaji wa mitalaa hiyo ni fursa pekee kwa wananchi mikoa ya nyanda za juu kusini hususani kwa vijana wasio na ajira kupata elimu ya biashara katika nyanja mbalimbali ambazo wataweze kujiajiri,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema uwekezaji huo wa Serikali ni mkubwa na umefika wakati wawekezaji nyanda za juu kusini wawatumie wataalamu wanaozalishwa katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

“Kama Serikali, tunao ushahidi  chuo cha CBE kinazalisha wataalamu wazuri katika nyanja mbalimbali na uwepo wa mitaalaa mingine ya ugavi, ununuzi na uhasibu itakuwa njia pekee ya kuwakomboa wawekezaji kufanya vizuri katika suala la uendeshaji wa biashara na kuepuka kukwepa kodi na hoja za wakaguzi wa hesabu,” amesema.

Homera amesisitiza wananchi kukiunga mkono chuo hicho ili kutimiza malengo ya Serikali ikiwemo ujenzi wa bwalo lenye uwezo wa kuchukua watu 1,000 na kuondoa adha ya wanafunzi na watumishi kutembea umbali wa kilometa tatu kupata huduma.

Related Posts