Serikali yataja sababu ya kumtimua Kiboko ya Wachawi

Dar es Salaam. Serikali imeweka wazi sababu ya kumfukuza nchini Kiongozi na Mchungaji wa Kanisa la Christian Life, Domique Dibwe maarufu kama Kiboko ya Wachawi, ikiwemo kukiuka misingi na mafundisho ya vitabu vitakatifu.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 7, 2024 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni wakati akifunga makambi yaliyoandaliwa na Kanisa la Waadventista Wasabato Maranatha lililopo Mtaa wa Maji ya Chai wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Masauni ametoa wito kwa wahubiri wengine kufuata mafundisho ya vitabu vitakatifu na sheria mbalimbali za nchi zinazosimamia taasisi hizo za kidini, huku akikemea matukio ya mauaji na ulawiti yanayoendelea nchini.

Julai 25, 2024 Serikali ililifungia kanisa la Kiboko ya Wachawi lililokuwa Buza, wilayani Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam likidaiwa kukiuka taratibu za usajili pamoja na kulifutia usajili kanisa hilo.

Baada ya kufungwa kwa kanisa hilo, mchungaji huyo aliondoka nchini kurudi kwao DRC tangu Julai 29, 2024 ambako anaendeleza huduma ya maombi hivi sasa.

Julai 25, 2024 Serikali ililifungia kanisa hilo lililokuwa Buza, wilayani Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam likidaiwa kukiuka taratibu za usajili. Kwa sababu hiyohiyo, Serikali ilifuta usajili wa kanisa hilo.

Katika barua ya kufutwa usajili wa kanisa hilo iliyotolewa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ilitaja suala la kutoza fedha kuanzia Sh500,000 kwa waumini ili awape huduma ya uponyaji wa kiroho, akisema inakiuka matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria mbalimbali Namba 3 ya Mwaka 2019.

Mbali na kutoza fedha, sababu nyingine za kufutwa usajili wa kanisa hilo zilizotajwa katika barua hiyo ni kutoa mafundisho yenye kuleta taharuki katika jamii na mahubiri ambayo ni kinyume cha maadili, mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania.

Baada ya kufungwa kwa kanisa hilo, mchungaji huyo aliondoka nchini kurudi kwao DRC tangu Julai 29, 2024.

Akizungumza Agosti mosi, 2024, Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, Paul Mselle alisema uwepo wa kiongozi huyo nchini umekoma baada ya kufutwa usajili wa kanisa lake.

Related Posts