Championship kuna vita nzito | Mwanaspoti

KILA msimu wa Ligi ya Championship inazidi kuwa tamu, ubora unaongezeka na hata wafuatiliaji wanaongezeka pia.

Ligi hiyo inashirikisha timu 16 ambazo kwa sasa ziko mkao wa kula zikisubiri kuanza msimu mpya wa 2024/25 mwishoni mwa mwezi huu na vita itakuwa ni kuwania kupanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026.

Kuna mzuka mwingi katika ligi hiyo kutokana na uwekezaji uliofanywa na timu hizo na kila moja ina hamu ya kucheza Ligi Kuu Bara, ili kuzidi kujiimarisha kimaslahi kutokana na fedha za wadhamini na kutengeneza jina hasa zile za nje ya Dar es Salaam.

Uwekezaji huo ndiyo umeifanya ligi hiyo ya pili kwa ukubwa nchini kuongezeka thamani kuliosababisha pia kuwa na ushindani, na inaelezwa msimu huu unaotarajiwa kuanza baadaye mwezi huu utakuwa mgumu hasa kutokana na usajili uliofanywa na timu hizo.

Tofauti na Ligi Kuu Bara, unaweza ukatabiri ni timu gani zitamaliza nafasi za juu kuanzia bingwa hadi nafasi ya nne, huku kwenye Championship ni ngumu na hadi ligi inapokaribia kumalizika ndio huanza kuonekana timu zitakazopanda daraja.

Msimu uliopita hadi mechi ya mwisho ndipo timu iliyopanda daraja ilijulikana.

Msimu ujao unatarajiwa kuwa na mambo mengi yatakayobamba na hapa Mwanaspoti linakuletea baadhi ya matukio yatakayonogesha zaidi ligi hiyo ambayo zamani ilijulikana kama Ligi Daraja la Kwanza.

MTIBWA, GEITA ZAKOLEZA MOTO

Mtibwa Sugar baada ya kukipiga kwa misimu mingi Ligi Kuu Bara, msimu huu itacheza Ligi ya Championship baada ya kushuka daraja msimu uliopita sawa na Geita Gold iliyoshuka nayo na kuzipisha Pamba Jiji na KenGold.

Hakukuwa na namna baada ya kuwa na msimu mbovu ligi kuu na sasa miamba hiyo inaonekana kujipanga hasa kuhakikisha zinarudi ligi kuu.

Hii ni kutokana na namna zilivyosajili lakini ni wazi haitakuwa kazi rahisi kuchuana na miamba mingine 14 kwenye ligi hiyo.

Zimejipanga kuanzia kwenye mabenchi ya ufundi na wachezaji waliosajili na kwa asilimia kubwa wametoka ligi kuu na wale wenye uzoefu na ligi hiyo na kwa sasa zinasubiri tu kipenga cha kuanza ligi zikaone yaliyomo yamo kwani wanasema ligi hiyo si mchezo na usipokuwa makini unabaki hapo hapo.

Kitu kingine kitakachonogesha ligi hii ni uwepo wa mastaa wengi waliowahi kutamba Ligi Kuu Bara.

Anuary Jabir aliyewahi kuwika na Dodoma Jiji, yuko Mtibwa Sugar pamoja na Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Amani Kyata, Erick Kyaruzi, George Makang’a, Costantine Malimi. Pia wapo Paul Godfrey ‘Boxer’ na mastaa wengi ambao wanainogesha ligi hiyo.

Kwa upande wa Geita Gold itakuwa na Aron Kalambo aliyekuwa Dodoma Jiji, beki Frank Magingi aliyekipiga Namungo. Pia imesajili staa wa kigeni, Fabrice Kayembe raia wa DR Congo na Adeyum Saleh, Abdulaziz Makame, Andrew Simchimba.

Hapa ndipo pa kuzikumbusha timu ngeni kwenye ligi hiyo, Mtibwa Sugar na Geita Gold huku hakuna ukubwa, ukizubaa watakushangaza na kila moja inakuwa na tahadhari kwa mwenzake.

Ni wazi ugumu wa ligi hii unazifanya timu kutokuwa na uhakika wa moja kwa moja wa kupata ushindi na mambo ya kushangazana ni kawaida baada ya dakika 90.

Hivyo hata, Geita Gold na Mtibwa Sugar hazitakiwi kujiamini sana zisije zikaangukia pua kama ilivyotokea kwa Biashara United na Ruvu Shooting na tangu zishuke hazijarudi Ligi Kuu Bara.

Kwa taarifa yako ni kwamba makocha ‘Wazungu’ hawaishii tu ligi kuu, kwani hata huku Championship wapo.

Mzungu wa Championship ni Melis Medo raia wa Marekani ambaye amekabidhiwa mikoba ya kuifundisha Mtibwa Sugar ya Morogoro. Medo atakuwa na kazi ngumu sana ya kupambana na makocha wenzie kama Mohammed Kijuso, Amani Josiah, Ivo Mapunda na wengineo kuwania nafasi ya kupanda ligi kuu kwa msimu ujao.

Kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hii, zipo ambazo ni wazi zitafuatiliwa zaidi, lakini hapa nakusihi uzifuatilie hizi; Biashara United na Mbeya Kwanza.

Kwa nini? Ni wazi zinaonekana kuwa ‘vigogo’ wa ligi hii na msimu uliopita ziliteleza kidogo kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kucheza ‘play off’ na kufeli.

Ndizo timu za kutazamwa zaidi msimu ujao licha ya uwepo wa Mtibwa Sugar na Geita Gold ambazo nazo zimejipanga hasa na ni wazi pia zitatupiwa jicho kuona zitafanya nini.

Pia kuna Songea United, TMA Stars na Polisi Tanzania kwani nazo zimejipanga hasa kwenye usajili wa wachezaji wazuri na watakaoifanya ligi kuwa tamu.

Uhondo mwingine wa ligi hiyo ni uwepo wa dabi nyingi  zitakazokoleza ushindani na kuna zile za Kanda ya Ziwa zinazozihusu Biashara United na Geita Gold. Pia kuna dabi ya jeshi na zipo TMA Stars, Polisi Tanzania na Green Warriors na ile dabi ya Arusha na kuna TMA na Mbuni FC.

Related Posts