Morogoro. Miili ya watu wawili kati ya wanne waliofariki kwenye ajali iliyohusisha magari matatu mkoani Morogoro, imetambuliwa ambapo dereva wa basi lililosababisha ajali hiyo tayari ameshakamatwa na anaendelea kuhojiwa.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Septemba 7, 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Yohana Mjengi ametaja majina ya miili iliyotambuliwa kuwa ni Pius Mkude (25), dereva wa Fuso na mkazi wa Dar es Salaam na Kenneth Sinyinza (49), mwanajeshi na mkazi wa Dodoma.
Kaimu kamanda huyo pia amemtaja dereva aliyekamatwa kwa tuhuma za kusababisha ajali hiyo kuwa ni Simon Hassan, mkazi wa Kihonda, Morogoro aliyekuwa akiendesha basi la abiria lenye namba za usajili T440 DNN aina ya Yutong, mali ya kampuni ya Kibasa lililokuwa likitokea Morogoro kwenda Dar es Salaam.
“Hili basi, likiwa linalipita gari jingine bila kuchukua tahadhari, lililigonga gari aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T896 DHM lililokuwa likiendeshwa na dereva, Pius Mkude ambaye sasa ni marehemu likitokea Dar es Salaam kuelekea Morogoro.
“Baada ya hapo, basi hilo lilipoteza uelekeo na kugonga gari lenye namba za usajili T 405 EBD Toyota Wish iliyokuwa ikiendeshwa na Keneth Sinyinza, mwanajeshi ambaye ni mmoja wa waliofariki katika ajali hiyo,” amesema Kamanda Mjengi.
Kufuatia ajali hiyo, Kaimu Kamanda huyo amewataka madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka matukio ya ajali zinazoweza kuepukika.