Polisi yaanza uchunguzi kada Chadema anayedaiwa kutekwa kwenye basi

Dar es Salaam. Wakati Chadema ikidai kutekwa Mjumbe wa Sekretarieti ya chama hicho Taifa, Ally Mohamed Kibao akiwa kwenye usafiri wa umma, Jeshi la Polisi limesema limeanza uchunguzi kubaini kilichotokea, chanzo chake na watu waliohusika.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime leo Septemba 7, 2024 imesema jana Septemba 6, 2024 zilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa jioni maeneo ya Tegeta jijini Dar es Salaam, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Ally Mohamed Kibao, akiwa safarini na basi la Tashrif alichukuliwa na kushushwa kutoka kwenye basi hilo na watu ambao hawakuweza kujulikana majina yao.

“Leo Septemba 7, 2024 tumesikia taarifa kuhusiana na tukio hilo kupitia vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, John Mnyika.

“Jeshi la Polisi, lingependa kutoa taarifa kuwa, lilipokea taarifa hiyo na kuanza uchunguzi wa kubaini kilichotokea, chanzo chake na watu waliohusika ni kina nani,” imesema taarifa ya Polisi.

Mnyika akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 7, amesema taarifa za tukio hilo zilianza kusambaa Septemba 6  kupitia mitandao ya kijamii ikidaiwa saa 12.00 jioni Mohamed akiwa kwenye basi la abiria la Kampuni ya Tashrif akitoka Dar es Salaam kwenda Tanga eneo la Kibo Complex Tegeta basi lao lilizuiwa na magari mawili.

Katika magari hayo yaliyozuia basi hilo, inadaiwa watu wenye silaha walishuka na kupanda ndani ya basi hilo na kumkamata kisha kumfunga pingu.

Mnyika akizungumza jijini Dar es Salaam amesema taarifa walizopata kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo, basi alilopanda Mohamed lilizuiwa na magari mawili ambayo hayakuwa na nembo yoyote kuonyesha yapo chini ya chombo gani cha dola.

Anadai watu walioshuka kwenye magari hayo walikuwa na silaha na kwamba mmoja alikwenda mbele ya kioo cha dereva na kumuamuru asiondoe gari.

“Wawili waliingia ndani ya gari na wengine walibaki nje, walioingia ndani walikwenda moja kwa moja alipokaa mzee Ally na kumchukua kwa nguvu na wakati wakiondoka aliongezeka mtu mwingine ambaye inaonekana alikuwa ndani ya basi kwa kivuli cha abiria na kuungana na watu wenye silaha na kuondokana nao, lakini pamoja na kumchukua kwa nguvu walimpiga wakimchukua,” amedai.

Mnyika amedai wakati watu hao wakimchukua mzee Ally kwa taarifa walizopewa walionekana ni kama vyombo vya usalama lakini baada ya ufuatiliaji watu hao hawakujitambulisha ni kina nani.

Mnyika amesema bado hawafahamu mzee huyo alipo na tayari wamemtuma wakili wa chama makao makuu ya Jeshi la Polisi ili kama Jeshi hilo ndilo linamshikilia likiri kufanya hivyo.

Amewataka mawakili wa Chadema kutafakari tukio la kukamatwa kwa Mohamed, ambalo anadai lina viashiria vyote vya vyombo vya usalama nchini kuhusika.

“Katika hili suala la mzee Ally Kibao lifungue ukurasa wa mapambano mahakamani wa kutafakari sasa iwapo ni sahihi kulishtaki Jeshi la Polisi peke yake,” amesema.

Mnyika pia ametaka mmiliki wa mabasi ya Tashrif ambalo mzee Ally alipanda kutoa tamko na taarifa juu ya abiria anayedaiwa kuonekana akishirikiana na watu walioondoka na mzee huyo.

Kwa kutumia taarifa zilizopo kwenye tovuti za kampuni ya mabasi ya Tashrif, namba ya simu iliyowekwa ilipopigwa mtu ambaye hakutaja jina amesema hana taarifa ya kukamatwa kwa kiongozi wa Chadema ndani ya basi lakini atazifuatilia na kutoa taarifa.

“Kwa sasa nipo Mombasa (Kenya) hizo taarifa sijazipata nitazifuatilia halafu nitatoa taarifa,” amesema.

Namba hiyo ya simu inasomeka kwa jina la Tashrif Bus Service.

Related Posts