Morogoro. Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama kuu Morogoro, Fadhili Mbelwa amewaapisha jopo la majaji saba ambao watakuwa na kazi ya kupitia kazi na kupata washindi Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) za mwaka 2023 zinazofanyika mwaka huu.
Tuzo hizo zinaandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), kazi zilizowasilishwa ni 1,135 za waandishi nchini na kupokewa ambapo kwa mara ya kwanza zitafanyika Septemba 28 mwaka huu mkoani Morogoro.
MCT ikishirikiana Mwananchi Communications Limited (MCL) watatoa tuzo ikilenga kumuenzi, mwandishi wake mkongwe, Zephania Ubwani aliyefariki duniani Aprili 6, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 7, 2024 mjini Morogoro, Katibu Mtendaji wa MCT na Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo EJAT mwaka 2023, Ernest Sungura amesema amesema vipengele vinavyowaniwa ni 19.
Sungura amesema Baraza la Habari Tanzania ikishirikiana na Mwananchi Commucations kutoa tuzo ambazo zinaenda sambamba kumuenzi mwandishi mkongwe, Zephania Ubwani kama ishara ya kuenzi uandishi wa utaalamu maalumu (Specialization) ambapo wakati wa uhai wake Ubwani aliuishi na kuutimiza.
“Kumekuwa na mwamko mkubwa kwa waandishi wa habari kuwasilisha kazi zao ili ziweze kushindanishwa tofauti na miaka minne iliyopita ambapo mwaka 2020 ni zilikuwa kazi 396, mwaka 2021 ziliongezeka na kufikia 608 huku mwaka 2022 kazi zikiwa ni 893. Hii imetokana na mifumo ya uwasilishwaji kurahisisha zaidi ikiwemo njia ya kidijitali,” amesema Sungura.
Sungura amesema waandishi wa Mkoa wa Dar es Salaam wameongoza kuwasilisha kazi nyingi (290) wakifuatiwa na Mkoa wa Arusha 81, Mwanza 74, Iringa 72 na Mtwara ikiwa na kazi 49 na upande wa Zanzibar zimepokelewa kutoka Kaskazini Pemba 36, Kusini 43 na Mjini Magharibi 29.
Aidha waliopishwa kuwa majaji ni Absalom Kibanda, Halima Shariff, Esha Muhidin, Jenifa Sumi, Mkumbwa Ally, Halima Msellem na Egbert Mkoko.
Mwenyekiti wa Jopo la Majaji EJAT 2023, Halima Shariff amesema kazi yao ni kutenda haki katika ujaji wao kwa kuangalia vigezo 16 vilivyowekwa na MCT katika kujaji kazi zilizowasilisha katika kupata washindi.
Umahiri wa waandishi wa habari na madhumuni kiujumla, kuibua vipaji vya waandishi wa habari, kuimarisha uledi na kujenga tasnia ya habari, kuangalia taarifa zinazojenga nchi na uweledi usiopasua umoja wa kitaifa na kuwatunza washindi kwa umahiri wao katika kujenga taifa la Tanzania.