Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga ameeleza fursa ambazo Tanzania imepata kupitia ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki.
Katika ziara hiyo ya Rais Samia nchini Uturuki iliyofanyika Aprili 17 hadi 21, 2024, Tanzania na Uturuki zimetiliana saini mikataba sita ya ushirikiano itakayochochea ukuaji wa wa uchumi kwa pande zote.
Rais Samia alifanya ziara ya Uturuki kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdoğan ikiwa ni miaka 14 tangu Rais wa Tanzania alipokwenda katika ziara ya kiserikali.
Balozi Ulanga amefafanua hayo leo Aprili 30, 2024 wakati wa mjadala wa Mwananchi X-Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa lengo la kuchambua safari ya kihistoria ya Rais Samia nchini Uturuki.
Balozi Ulanga kupitia mjadala huo ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu, amesema thamani ya ziara ya aliyoifanya Rais Samia ni kuainisha maeneo ya ushirikiano yanayoweza kuleta manufaa kwa Tanzania na Uturuki.
Katika mikataba iliyosainiwa, Balozi Ulanga amesema maeneo matatu yalizingatiwa ikiwamo elimu, eneo ambalo Uturuki imepiga hatua kwa kuwekeza katika ngazi mbalimbali ili kuwa na watumishi na wananchi wenye viwango vya juu wa ujuzi.
“Katika hayo matatu moja ni ufadhili kwa wanafunzi wa Kitanzania kupata fursa ya kwenda kusoma vyuo vikuu vya Uturuki na hati nyingine ni kuhakikisha wakufunzi wetu wa ngazi mbalimbali wanapata fursa za kuongeza ujuzi kwa kubadilisha uzoefu au kufanya tafiti na machapisho ya taaluma,” amesema.
Kupitia makubaliano hayo, amesema wanafunzi wa Tanzania watapata fursa za masomo nchini Uturuki na hati nyingine ni kuhakikisha wakufunzi wa ngazi mbalimbali wanapata nafasi za kuongeza ujuzi.
Hati ya nne ni eneo la uwekezaji iliyohusisha Kituo cha Uwekezaji (TIC) ikihusisha namna ya kuongeza uwekezaji kutoka Uturuki nchini Tanzania.
Balozi Ulanga amesema hati hiyo ni kuona namna ambayo nchi ya Uturuki inawatambua na kuwapa huduma stahiki inayofanya wananchi hao kurudi kufanya utalii.
Balozi Ulanga amesema makubaliano kwenye sekta ya elimu kuna eneo la ufadhili wa masomo na ipo namna ya kuangalia vigezo vinavyohitajika kwa ajili ya wanafunzi na vyuo watakavyokwenda kusoma hatua itakayoratibiwa na Wizara ya Elimu kutoa utaratibu mzima.
“Wizara za Elimu za Tanzania Bara na Zanzibar zitakuja na utaratibu mzima, suala la elimu lina mwingiliano wa moja kwa moja, watu wangependa kusoma katika vyuo vikuu vya Uturuki, hivyo katika mwaka ujao wa fedha tutaanza kupata taarifa kwenye vyombo vya habari kuhusu fursa za elimu nchini Uturuki,” amesema Balozi Ulanga.
Amebainisha kwamba mwaka ujao wa fedha, fursa za elimu nchini Uturuki zitaanza kutangazwa.
Kuhusu shahada ya heshima aliyotunukiwa Rais Samia na Chuo Kikuu cha Ankara, Balozi Ulanga amesema ni kutokana na kutambuliwa kwa mchango wa hali ya juu ambao umeutoa kwenye uchumi wa Tanzania.
“Shahada hiyo hutokana na utashi wa chuo kikuu na shahada hiyo haiombwi, chuo chenyewe kwa utashi wake kinaona fulani anastahili na wakishaona anastahili wanajenga hoja ambayo lazima ikubalike na seneti ya chuo na baraza, ndio baadaye hutolewa,” amesema.
Amesema shahada aliyotukiwa Rais Samia na Chuo Kikuu cha Ankara ni kutambua na kuthamini mchango wake katika kufanya mabadiliko ya uchumi nchini.
“Kumekuwa na mabadiliko ya uchumi ambayo yameifanya Uturuki kuwa miongoni mwa nchi 20 bora za uchumi mkubwa duniani. Kwa hiyo ni heshima tumeipata kama nchi, lakini ni heshima aliyopewa Rais Samia kwa kutambua na kutathmini mabadiliko makubwa ya uchumi anayoyafanya nchini,” amesema.
Akizungumzia hati za elimu, Waziri wa Elimu na Mafunzo Zanzibar, Leila Mohamed Mussa amesema hati zote walizosaini zina ufadhili wa elimu.
Amesema lengo la makubaliano hayo ni kuwajengea uwezo waajiriwa katika vyuo vikuu kwa kuwapatia ufadhili wa masomo ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu.
Kwa vyuo vya kati, amesema makubaliano hayo yatatoa fursa kwa wanataalamu waliopo nchini kuongeza taalamu zao.
“Lakini itasaidia kupata uzoefu kutoka kwa wenzetu namna walivyoweza kufanikiwa katika eneo hilo, kwa sasa wizara zetu zinaandaa mpango kazi wa kulitekeleza.
Kwa upande wa Zanzibar, amesema hati nyingine waliyosaini ya Zanzibar pekee ambayo ni maalumu kwa mwanafunzi aliyemaliza shule atapata fursa ya kuomba ufadhili uliotangazwa kupitia taasisi husika.
Amesema lengo la ufadhili uliosainiwa kwa upande wa Zanzibar ni kwa ajili ya wanafunzi waliofaulu vizuri katika mtihani wa kidato cha sita.
“Kwa hiyo, mwanafunzi akimaliza kidato cha sita, akifaulu vizuri katika masomo ya sayansi atapata ufadhili wa asilimia 100 kusoma vyuo vikuu vikuu vya Uturuki katika ngazi ya shahada, ni maalumu kwa wanafunzi 50 watakaofaulu vizuri,” amesema.