Visa, mikasa ndoa za ukewenza, namna ya kuishi kwa amani

Dar es Salaam. Ingawa baadhi ya imani za kidini na mila zinaruhusu ndoa ya zaidi ya mke mmoja, wivu, mashindano na visasi vimekuwa vikionekana kama vikwazo kwa baadhi ya wanawake kuingia kwenye aina hii ya ndoa.

Ripoti ya Utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) ya mwaka 2020/21, iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Januari 16, 2024, inaonyesha kupungua kwa idadi ya ndoa za zaidi ya mke mmoja ikilinganishwa na ripoti ya mwaka 2014/15.

Ripoti hiyo, iliyohusisha kaya 4,164, inaonyesha kwamba ndoa za mke zaidi ya mmoja zimepungua kutoka asilimia 6.4 mwaka 2014/15 hadi asilimia 2.0 mwaka 2020/21, ikiwa ni upungufu wa asilimia 4.4.

Kwa mujibu wa ushuhuda wa wanaoishi katika ndoa hizi, mabadiliko ya tabia ya waume baada ya kuoa mke wa pili ndiyo chanzo kikuu cha matatizo.

Hata hivyo, mtazamo huu unakinzana na ule unaoweka lawama kwa wanawake, ambao mara nyingi hutajwa kusababisha matatizo kwa kufuatilia maisha ya wake wenzao.

Hivi karibuni, tukio liliibuka kwenye mitandao ya kijamii la mwanamke mmoja mkazi wa Dar es Salaam kumwagiwa mafuta ya moto mikononi na mke mwenzake (bi mdogo), chanzo kikidaiwa kuwa ni mume kukataa kwenda kulala kwa mdogo kwa miezi kadhaa, jambo lililozua migogoro.

Viongozi wa dini wanasema ombwe la elimu juu ya namna ya kuishi katika ndoa ya mke zaidi ya mmoja linaweza kuwa moja ya chanzo cha changamoto hizo.

Wameeleza kuwa baadhi ya wanaume huingia kwenye ndoa hizi bila uelewa wa kina wa wajibu na haki zao kwa wake zao.

Hata hivyo, viongozi hao wanasisitiza kuwa ndoa ya mke zaidi ya mmoja yenye amani, furaha, upendo na masikilizano baina ya wake inawezekana na ina faida zake.

Ramla Othmani, ambaye ameolewa kama mke wa pili katika ndoa ya ukewenza, anasema mwanzoni alihisi hofu ya kuingia katika ndoa hiyo, akidhani atakutana na maisha ya malumbano.

Hata hivyo, alikubali kutokana na upendo wake kwa mumewe. “Hata familia yangu haikuwa tayari, lakini kwa kuwa nilionyesha nia, iliwalazimu kunipa baraka zao,” anasema.

Ramla anasema sasa ni miaka minne tangu aolewe, na ndoa yao ina amani na furaha. Kila mke anaishi maisha yake, ingawa wanawasiliana na kushirikiana katika mambo ya kifamilia yanayowahitaji kufanya hivyo.

“Nilichogundua kwa muda niliokaa kwenye ndoa ya aina hii ni kwamba tabia ya baadhi ya wanawake kutaka kufuatilia maisha ya mwenzake na kujua kila kinachoendelea ni moja ya sababu zinazochochea mifarakano,” anasema.

Naye Rashid Shabani, mume wa wake wawili, anasema sababu nyingine inayochangia mifarakano ni baadhi ya wanawake kupenda kusikiliza maneno ya watu wa nje bila kufanya uchunguzi.

Akizungumza na Mwananchi, Fatma Mdidi, mmoja wa watoa mihadhara ya dini ya Kiislamu kwa wanawake na mwalimu wa masomo ya Sayansi na Dini, anasema mitazamo ya jamii kuona ukewenza kama vita ni moja ya sababu za watu kuogopa kuingia katika ndoa za aina hii.

Mdidi, ambaye amekuwa katika ndoa ya mitala kwa miaka 17, anasema mtazamo huo unatokana na yale wanayoyaona au kuyasikia kuhusu visa na mikasa ya ndoa za ukewenza zilizotangulia.

“Kwa mfano, mtu aliyelelewa kwenye ndoa ya ukewenza yenye misuguano ni vigumu kumuelimisha kuwa ukewenza unaweza kuwa wa amani, kwa sababu amekuwa akiona mifarakano, ugomvi na vita katika familia, na hivyo kujengeka akilini mwake,” amesema Mdidi.

Anasema hiyo inafanya baadhi ya wanawake wanaoolewa ukewenza waanze kujiandaa kisaikolojia wakidhani ukewenza ni ugomvi tu kila kukicha, wakati kumbe wanaweza kuishi kwa amani, upendo na furaha.

Akieleza namna anavyoishi kwenye ndoa hizo za mitala, anasema kikubwa kilichomsaidia ni kuzaliwa na kulelewa kwenye familia yenye wakewenza.

“Ukewenza kwetu umeanzia kwa baba wa mama yangu, yaani babu yangu, na waliishi nyumba moja na watoto na hawakubaguana,” anasema Fatma na kuongeza:

“Lakini hata baba yangu aliwahi kuoa wake wawili, baba zangu wadogo pia, hivyo ni maisha ambayo nilishayazoea na tulikuwa tukiishi kwa amani.”

Mdidi anasema kuwa migogoro katika ndoa za mitala mara nyingi husababishwa na mwanamume mwenyewe anapokosa kutumia hekima katika mchakato wa kuoa mke wa pili.

Anasema baadhi ya wanaume huamua kuoa mke mwingine kwa kueleza mapungufu ya mke wa kwanza kwa mwanamke anayetarajia kumuoa.

“Huyu anayeolewa anaingia kwenye ndoa akiwa na taarifa kuhusu mapungufu ya mke aliyemkuta, na hivyo anaweza kujiona kama amepewa jukumu la kurekebisha mapungufu hayo, bila kujua kuwa naye pia ana mapungufu yake,” amesema.

Hali hii inaweza kusababisha mke mpya kumuona mke wa kwanza kama mtu aliyeshindwa, jambo ambalo linaweza kuibua kiburi na dharau.

Kwa upande mwingine, mke wa kwanza anaweza kujibu kwa kuonyesha kuwa bado hajashindwa, na hivyo kuzua migogoro kati yao.

Mdidi pia anabainisha kuwa kosa jingine linalofanywa na baadhi ya wanaume wanapooa mke zaidi ya mmoja ni kupunguza upendo kwa mke wa kwanza, jambo linaloweza kuongeza migogoro zaidi.

“Baadhi ya wanaume wanapoongeza mke hubadilika, huhamisha upendo kwa mke mpya aliyemuoa, hili linamfanya aliyetangulia kuwa mnyonge na kuona mke aliyeongezwa kama chanzo cha kutoweka upendo kati yake na mumewe.”

“Kwa kuwa bado anampenda mumewe huanza kimpambania na kila mtu ana namna yake ya kuliendea jambo hilo, hapo ndipo wakati mwingine huwa chanzo cha migogoro katika familia yenye mke zaidi ya mmoja,” amesema.

Anaongeza kuwa sababu hizo zinatokana na mambo makuu mawili: imani duni na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu ndoa ya ukewenza.

Ndoa ya ukewenza yenye amani inawezekana ikiwa haya yatafanyika:

Mdidi anasema kuwa ndoa ya uke wenza yenye amani, furaha, na maelewano inawezekana, akitoa mfano wake mwenyewe ambapo ametimiza miaka 17 katika ndoa ya ukewenza.

Kwa upande wa wanawake, amewashauri kuishi maisha yao na kutojishughulisha na maisha ya mke mwenzao.

Anasema kufuatilia mambo kama mke mwenzio amekula nini, amenunua nini, au ameenda wapi ni moja ya vyanzo vikuu vya migogoro na malumbano.

Pia anasisitiza kuondoa dhana potofu kuwa wanawake wanaoingia katika ndoa ya ukewenza lazima wagombane.

Kwa upande wa wanaume ambao wameoa wake zaidi ya mmoja, anawataka kufanya uadilifu kama dini inavyobainisha, kwani kufanya hivyo kutasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

Kwa upande wake, Sheikh Yakub Ndembo anasema chanzo kikubwa cha migogoro hiyo ni ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu ndoa na misingi yake.

Anaeleza kuwa ukosefu wa elimu ya kutosha miongoni mwa wanandoa husababisha kuibuka kwa migogoro, mara nyingi kutokana na ndoa hizo kutoongozwa na mafunzo sahihi ya dini.

“Ukweli ni kwamba siku hizi ndoa nyingi za matala haziongozwi na mafunzo sahihi ya dini; badala yake, kila mmoja huziendesha kwa namna anavyoona inafaa na kwa matashi yake, hivyo kukosa mizani ya uadilifu na haki,” anasema Sheikh Ndembo.

Anasisitiza kuwa ili ndoa hizo ziwe na amani, ni muhimu elimu kuhusu ndoa na maadili yake iendelee kutolewa, hasa kwa vijana.

“Kukosekana kwa elimu ya kutosha miongoni mwa wanandoa imekuwa chanzo cha migogoro katika ndoa nyingi,” anasema.

Related Posts