Ishu ya Kagoma, Simba ipo hivi!

MASHABIKI wa Simba wametaharuki baada ya kuzagaa taarifa kwamba kiungo mkabaji mpya wa timu hiyo, Yusuf Kagoma amepigwa stop, lakini ukweli ulivyo juu ya sakata hilo haupo hivyo baada ya menejimenti ya mchezaji na mabosi wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya TFF kuanika kila kitu.

Kagoma aliyesajiliwa na Simba kutoka Singida Fountain Gate, baada ya awali kuhusishwa na Yanga, na kesi yake kufikishwa TFF ambako awali ilionekana kama imeisha, lakini mambo yamebadilika baada ya mabosi wa Jangwani kucharuka na kurudisha tena faili TFF, na juzi kesi ilisikilizwa ila haijatolewa hukumu.

Kutokana na kuitishwa kwa shauri hilo, mitandaoni na vijiweni kulikuwa na taarifa kwamba Kagoma kazuiwa kuitumika Simba hadi atakapomalizana na Yanga, huku wengine wakienda mbali kwamba Mnyama atapoteza pointi kwa kumtumia mchezaji asiye halali katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara zilizopita.

Sakata lilipoanzia. Ilikuwa ni mara baada ya dirisha la usajili kufunguliwa katikati ya mwaka huu, Yanga ilimalizana na Fountain Gate (zamani Singida FG) ili kumsajili Kagoma na walituma fedha walizohitaji, lakini kabla ya mchakato kukamilika inaelezwa Simba nayo ilituma fedha ili kumbeba kiungo huyo na dau lao lilikuwa kubwa zaidi.

Inaelezwa, mabosi wa Fountain walimuita Kagoma na kumuuliza anataka kwenda wapi baada ya Yanga na Simba kila moja kupeleka kishika uchumba na kiungo huyo wa zamani wa Geita Golda aliichagua Simba na kutoa baraka zote aende, lakini hakuzirudisha fedha za Yanga kwa vile dili lilishakufa.

Inadaiwa mabosi wa klabu hiyo waliamua kumtumia mmoja wa vigogo aliye na ukaribu na Yanga na Singida Black Stars, ili ishu kumalizika na Jangwani alishaanza kuridhia, lakini kauli za kejeli zilizotolewa na watu wa Simba na menejimenti ya mchezaji ziliwakera na kurudisha faili tena TFF baada ya awali kukaushia.

“Unakumbuka wakati wa kesi za Awesu Awesu, Valentino Mashaka, la Kagoma nalo lilikuwapo na lilionekana mambo ni shwari ndio maana jamaa aliendelea kukipiga Simba, lakini kejeli wakati Yanga haijapewa fedha zao na walishakubaliana na klabu kwa usajili wa kiungo huyo imewachafua na kuanzisha upya kesi iliyosikilizwa juzi (Ijumaa),” kilifichua chanzo hicho bila kutaja fedha ambazo Yanga na Simba ilizitoa, ila ikielezwa dau la Simba lilikuwa kubwa zaidi na kuwavuruga mabosi wa Fountain Gate.

Hata hivyo, Mwanaspoti liliamua kuchimba ukweli wa mambo na kuelezwa picha nzima ilivyo, huku mwanasheria wa mchezaji huyo, Leonard Richard na viongozi wa Kamati ya Sheria ya TFF wakifunguka kwamba hukumu haijatoka na Simba wala haina tatizo katika sakata hilo la Kagoma.

Richard ameliambia Mwanaspoti kuna upotoshwaji mkubwa wa sakata la mchezaji huyo na kuhusishwa kwake na Simba.

Sintofahamu iliyoibuka kutokana na Kagoma kutumika katika mechi ya Simba wakati shauri lake likiwa bado halijatolewa uamuzi na kuelezwa timu hiyo inapaswa kukatwa pointi, ndipo Richard alipoibuka na kutoa ufafanuzi kuhusiana na sakata hilo.

“Kesi iliyopo Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji haihusiani na Yanga kuishtaki Simba, bali ni sakata baina ya uongozi wa Fountain Gate na Wanajangwani pamoja na Kagoma kuhusishwa, ndio maana mimi nasimamia kesi hii,” alisema Richard.

“Shida iliyopo ni mchezaji, Singida Fountain Gate na Yanga kwa upande wa Simba hawahusiki na ndio maana leseni ya mchezaji wanayo na anaendelea kucheza huko.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, Said Soud alisema jana hawajatoa uamuzi wowote kumhusu Kagoma zaidi wamewataka viongozi wa pande zote mbili kukaa na kumaliza suala hilo.

“Hakuna uamuzi tuliotoa kuhusu Kagoma, wenyewe tunashangazwa na taarifa zinazosambaa kuhusiana na sisi kutoa kauli ya kumtaka mchezaji asicheze. Kilichofanyika ni kuwaomba viongozi wa pande mbili walioleta kesi wamalizane,” alifafanua Soud na kuongeza, hatima ya Kagoma itafahamika kikao kijacho mara baada ya viongozi kukamilisha walichowaagiza wafanye ndipo watatoa majibu.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa Singida Fountain Gate ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alikiri ni kweli uongozi wa timu hiyo ulipokea fedha kutoka timu zote mbili, lakini Simba ndio walikuwa na dau nono na ndio maana mchezaji huyo alitua Msimbazi.

“Sakata lililopo lina ukweli lakini linatuhusisha sisi Fauntain Gate na Yanga kwani ni kweli tulipokea kiasi cha fedha kutoka kwao na baadae tukachukua Simba na kuwapa mchezaji,” alisema kiongozi huyo na kuongeza:

“Baada ya kumuuza mchezaji Simba mchakato wa kurejesha fedha Yanga haukufanyika hiyo ndio shida iliyopo nafikiri viongozi wa pande zote mbili tutakaa na kutatua shida hiyo ili kumpa wakati mzuri mchezaji kutumikia timu yake.”

Related Posts