Mbeya. Serikali imesema bado kuna dawa na vifaa tiba vyenye nembo ya Serikali zinazokamatwa kwenye maduka ya dawa na hospitali na maabara za watu binafsi zikiuzwa.
Inadaiwa baadhi ya wataalamu wa maabara huagiza vifaa tiba hivyo vyenye nembo ya Serikali na kuvifungia stoo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Aprili 18, 2024 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Nbeya, Elizabeth Nyema alipofungua mkutano wa wataalamu wa maabara na wafamasia wa ngazi ya vituo vya afya wa halmashauri na hospitali.
“Kuna wafamasia na wataalamu wa maabara wenye maduka ya dawa na hospitali binafsi si waaminifu, katika kaguzi mbalimbali dawa na vifaa tiba vya Serikali vinabainika kwenye maduka ya dawa na hospitali zao binafsi kinyume cha utaratibu,” amesema.
Aidha, Dk Nyema amewaagiza wataalamu wote wa maabara wakipokea vifaa tiba na dawa kuziwekea nembo maalumu kwa lengo la kuisaidia Serikali kukabiliana na changamoto hiyo katika kutoa huduma.
“TMDA imetekeleza majukumu yao kwa kupita kwenye maduka kufanya kaguzi, lakini bado kwa upande wa Serikali kuna changamoto, maduka ya wafamasia katika kaguzi wanabainika kuwa na vifaa tiba na dawa za Serikali kinyume cha utaratibu,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa TMDA, Dk Anitha Mshighati amesema wanaendelea kuimarisha udhibiti katika maeneo ya mipakani, ili kuhakikisha vifaa vinavyozalishwa na kuingizwa nchini viwe vimesajiliwa.
“Lengo ni kuona vifaa tiba vinavyoingizwa nchini na kuzalishwa kwenye viwanda kuwa na ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma, sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya kada ya wafamasia na maabara,”amesema.
Elizabeth Mashauri, msanifu wa vifaa tiba kutoka Hosptali ya Wilaya ya Kyela, amesema kuna changamoto hiyo kwa baadhi ya wafamasia kuwa na vifaa tiba na dawa za Serikali kinyume cha utaratibu na kutoa siri za kazi ya ukaguzi.
“Zamani TMDA walikuwa wakiwatumia wafamasia kuwapeleka kwenye maduka ya wauzaji wa dawa, lakini kuna vifaa tiba vya Serikali ambavyo muuzaji hana uwezo wa kutumia kutoa huduma kwa wagonjwa,” amesema.
Aidha, ameomba Serikali kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, ili kudhibiti matumizi holela ya vifaa tiba na dawa za Serikali katika hosptali na maduka binafsi.