Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema akizungumza na Mwananchi asubuhi ya leo Jumapili, Septemba 8, 2024 amesema familia ya Ali Kibao imejulishwa uwepo wa mwili unaofanana na Kibao katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyama, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Polisi wameijulisha familia ya Ally Kibao kuwa kuna mwili unaofanana na wa Ali Kibao upo Hospitali ya Mwananyama. Sasa familia na viongozi wanakwenda kufuatilia nini kinaendelea na undani wake,” amedai Mrema.
Kibao ambaye ni Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema anadaiwa jioni ya Septemba 6, 2024 maeneo ya Kibo Complex Tegeta jijini Dar es Salaam, akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga na basi la Tashrif alishushwa kwenye basi hilo na kuchukuliwa na watu wasiojulikana majina yao wala walipotokea.
Jana Jumamosi, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema wanafuatilia tukio hilo.
Misime alisema hivyo saa chache kupita tangu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuzungumza na waandishi wa habari na kutoa wito kwa vyombo vya dola kufuatilia tukio hilo.
Mnyika alidai katika magari yaliyozuia basi hilo, inadaiwa watu wenye silaha walishuka na kupanda ndani ya basi hilo na kumkamata kisha kumfunga pingu.
Viongozi wa Chadema, wakiongozwa na Freeman Mbowe kwa sasa wanaelekea Mwananyamala Hospitali.
Misime alipotafutwa na Mwananchi Digital leo Jumapili saa 4:35 asubuhi kuhusiana na suala hilo, simu yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyesema kuwa bosi wake yupo kwenye ibada.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi