BAADA ya kufuzu kucheza kombe la dunia kwa vijana wa chini ya miaka 19, Tanzania ina kibarua kingine cha kusaka tiketi ya kucheza fainali za kombe la dunia kwa kriketi ya mizunguko 20 ambayo Dar es Salaam ndiyo mwenyeji wake.
Ni michuano inayoshirikisha timu za mataifa sita ya Afrika ikiwemo Tanzania, kwa mujibu wa ratiba ya mashindano iliyotolewa na Chama cha Kriketi nchini, TCA kwa kushirikiana na chama cha kriketi duniani, ICC.
“Tuko tayari na vijana wameandaliwa vyema kwa mashindano haya. Naamini hatutawaangusha Watanzania,” amesema Ateef Salim ambaye ni afisa habari wa chama cha kriketi nchini, TCA.
Nchi nyingine zitakazoshiriki michuano hii ya kufuzu ni Cameroon, Ghana, Mali, Lesotho na Malawi.
Katika michuano ya vijana chini ya miaka 19, Tanzania iliibuka mshindi wa kwanza mbele ya Sierra Leone waliokuwa wa pili na NigerIa walioshika nafasi ya tatu.
Kwa kushinda mashindano hayo Tanzania pia ilipanda daraja kutoka divisheni ya pili na kuwa katika divisheni ya kwanza.
Katka mashindano haya, kwa mujibu wa ratiba ya mashindano, Tanzania itaanza mbio za kufuzu na Mali katika mchezo utakaopigwa Septemba 21 katika uwanja wa Dar Gymkhana jijini.
Siku hiyo hiyo, Lesotho watacheza na Malawi katika uwanja wa UDSM saa tatu asubuhi, na saa saba mchana, uwanja huo utaishuhudia Cameroon ikimenyana na Ghana.
Siku ya pili, Septemba 22 mwaka huu, Tanzania itakuwa kibaruani uwanja wa UDSM dhidi ya Lesotho baada ya kumalizika kwa mechi ya asubuhi kati ya Camertoon na Mali wakati uwanja wa Dar Gymkhana utakuwa shuhuda wa mechi kati ya Ghana na Malawi.
Tarehe 23 Septemba itakuwa ni siku ya mapumziko kabla ya timu kurejea tena uwanjani tarehe 24 Septemba.
Tanzania itakuwa na mechi yake ya tatu katika uwanja UDSM ikipambana na Cameroon wakati uwanja wa Dar Gymkhana utakuwa ukitimua nyasi kwa mechi kati ya Ghana na Lesotho, baadaye Malawi watakuwa wakikiwasha na Mali.
Tarehe 24 Septemba, Tanzania itakuwa tena katika uwanja wa Dar Gymkhana safari hii ikipambana na Ghana kabla ya Cameroon kuumana na Malawi majira ya mchana.
Tanzania itamaliza kibarua chake kwa kuikaribisha Malawi katika uwanja wa UDSM baada ya kumalizika kwa mechi kati ya Ghana na Mali, na mechi kati ya Cameroon na Mali ndiyo itakayofunga dimba la michuano katika uwanja wa Dar Gymkhana.