Vijiwe vya kahawa ni jungu kuu la kusaka busara kwa wanaume

Dar es Salaam. Kijana wa miaka 36 (jina linahifadhiwa) anaanza kwa kusema, “Nilipata changamoto kubwa ya kuiongoza familia yangu. Ilifikia hatua nilifikiria kuachana na mke wangu.

“Nilipozungumza na baba, aliniuliza maswali kadhaa, kama vile iwapo nimewahi kutafuta ushauri na kama kuna watu ninaoshirikiana nao kimtazamo na kushauriana.”

Kijana huyo anasema alimweleza baba yake jinsi anavyosikia simulizi nyingi akiwa na marafiki zake baa kuhusu wake zao au wapenzi wao, na namna wanavyomaliza changamoto hizo. Alijaribu kufuata ushauri alioupata kutoka kwao.

“Baba aliniambia sikuwa sahihi na kunishauri niende nyumbani Temeke wikiendi. Nilipofika, nilisalimiana na mama, kisha nikatoka na Mzee mpaka kwa rafiki zake kwenye kijiwe cha kahawa.

“Tulikaa pale kwa takriban dakika 50, ambapo mazungumzo yalihusu zaidi siasa, mpira na maisha. Katika mada ya maisha, kama vile aliwapanga, waliongea kuhusu maisha ya ndoa na jinsi mwanamume anavyopaswa kuishi na mke, watoto na familia.

“Mazungumzo yalipoisha, tuliondoka. Tulipofika nyumbani, baba akaniambia niende kwa mke wangu na watoto bila kusema chochote,” anasimulia kijana huyo anayeishi Mbezi, Dar es Salaam.

Anasema tangu siku hiyo alianza kutafuta kijiwe cha kahawa karibu na kwake, na sasa huenda mara kadhaa na kuzungumza na wazee.

“Kuna mambo mengi najifunza kila siku kwa watu wazima, na yameifanya familia yangu pia kuwa na furaha. Najitahidi kila wikiendi kukaa na wazee angalau nusu saa kabla ya kwenda kukutana na washkaji baa.”

Simulizi ya kijana huyu inaonyesha tatizo lililojificha katika jamii, ambapo baadhi ya vijana wamedharau vijiwe vya kahawa, wakidhani ni maeneo ya watu wasio na kazi au wanaojitenga na wenye kipato.Hata hivyo, baadhi ya wazee waliozungumza na gazeti la Mwananchi wanasema vijiwe vya kahawa vina manufaa mengi, kwani chimbuko lake lilianzia wakati wa harakati za uhuru, ambapo wazee walikutana kujadili masuala muhimu kwa Taifa.

Mzee Juma Awadh (72), mkazi wa Kivule, Dar es Salaam, anasema vijiwe vya kahawa vilikuwa chanzo cha mikakati mingi ya kimapinduzi.

“Mwalimu Julius Nyerere alianzisha harakati zake nyingi katika vijiwe hivi tunavyoviona sasa. Vijiwe vya kahawa vilikuwa sehemu ya kupanga mikakati, kutoa dira, na kuhamasisha.

Baada ya uhuru, wazee waliendeleza vijiwe hivi na sisi vijana wa wakati huo tulijumuika. Tulijifunza mengi na familia zetu zilistawi, lakini sasa naona vijana wanavipuuza,” anasema Awadhi.

Adam Kiyeyeu (61) anakumbuka jinsi vijiwe vya kahawa vilivyokuwa na taarifa zote muhimu. “Ukitaka jambo fulani au unahitaji kufikisha ujumbe kwa Rais, vijiwe hivi vilikuwa na maelekezo yote bila kukosea. Zamani, vilikuwa sehemu ya kutatua mambo magumu na kufanikisha mipango mikubwa,” anasema Kiyeyeu.

Licha ya kwamba vijana walio wengi hawajui umuhimu wa vijiwe vya kahawa, baadhi yao wanakiri kwamba hukusanya watu wa sekta zote, serikalini, walalahoi na watu binafsi na wote hutoa maoni ya kile kilicho sawa na kisicho sawia kwa wakati mmoja mkasikiliza na kujifunza.

“Ukiachana na uongo wa vijiwe hivi vya kahawa, pia kuna faida muhimu ya kujifunza kama kijana msomi na kiongozi wa baadaye nayo ni kujiamini,” anasema Jafari Omary (32), mkazi wa Vijibweni, Kigamboni.

Anasema kujiamini katika kile unachokizungumza wakati huo, haijalishi ni cha uongo au kina ukweli ndani yake, kuijenga hoja na kuitetea kwa wakati mmoja ndani ya kijiwe cha kahawa ni ustadi, nadhani wengi tunafahamu hili na limekuwa tatizo kwa walio wengi tu kiasi kuleta shida katika kazi zao,” anasema Jafari.

Hata hivyo, baadhi ya vijana walisema hakuna wanachoelewa katika vijiwe hivyo.

“Sijawahi kwenda huko na sioni umuhimu wake, inawezekana kwa sababu mimi kijana nakutana na taarifa nyingi mitandaoni, nikitaka ushauri nakaa na washkaji tunaongea. Ila naamini kwamba wazee wanaweza kukufahamisha zaidi sisi tunadanganyana tu,” anasema Erick (27).

Lameck Henry (42) anasema ingawa yeye si mhudhuriaji wa vijiwe vya kahawa, anaamini kuna mengi mazuri huko.

“Niliwahi kwenda mara moja nikagundua ukitaka wabobezi wa biashara yoyote unayotaka kuifanya kwa mtaji wako huo huo tembelea katika vijiwe hivi, muhimu tu usiwe na haraka katika jambo lako linalokutatiza, utafika tu wasaa wa kuzungumzia biashara, nawe hapo hapo utapata upenyo wa kuomba ushauri, japo huwezi kujisema kabisa kama ni wewe.

“Unaweza tumia hata mtu fulani au mtu wako wa karibu kama ndiye mhusika wa hicho anachotaka kwenda kukifanya,” anasema Lameck.

Licha ya kwamba kwamba kuna mitandao ya kijamii na makundi sogozi, yanayowafanya watu au hata wanaume wajumuike pamoja, vijiwe vya kahawa vimetajwa kuwa na umuhimu kwa wanaume.

Baada ya kushiriki katika moja ya kijiwe cha kahawa Kitunda Shule, Ilala jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, nilipata kujua mambo mengi kuhusu wanaume, hasa mmoja wao aliposimulia kuwa hupigwa na mkewe na kuhitaji ushauri.

Mwenyekiti wa kijiwe hicho, Joseph Haule ananiambia kuwa mada waliyoijadili ilihusu sababu ya mtoto kumpenda au kumpendelea mama zaidi huku baba akipewa kisogo.

“Ilikuwa ni mada mtambuka tukizungumzia masuala ya malezi kwa jamii, malezi kila pande baba, mama watoto kuna changamoto zake na kwa sababu ya hizo, kuna mambo mbalimbali ambayo yanaendelea kutokea na ambayo yanasababisha kuzaliwa kwa changamoto nyingine, kama tutaweza kuzitatua basi tutakuwa tumeweza kuisaidia jamii kupunguza hizo changamoto,” anasema.

Ameongeza kuwa walichokiona na kujifunza ni ukaribu wa mama kwa mtoto, jambo linalochangia kwenye nini kifanyike kwa sababu mwanzoni ndoa zilikuwa ni taasisi za kutengeneza jamii, lakini imefikia hatua ndoa imekuwa si taasisi ya kutengeneza jamii.

“Imekuwa matakwa ya mwanamke na mwanamume, tupo zama ambazo tamaa zetu binafsi zinatusukuma zaidi kutupeleka kwenye ndoa kuliko misingi yenyewe, kwa maana ya kuiendeleza kama taasisi ya kupata watoto.”

Haule anasema walimaliza mjadala huo kwamba kila mwanamume arudi kwenye misingi kutimiza jukumu la ndoa na malezi.

Mwezeshaji kutoka Mtandao wa Ushiriki wa Wanaume Tanzania (MenEngage Tanzania) Iddi Mziray anasema amekuwa akishiriki vijiwe mbalimbali vya kahawa na kuzungumza moja kwa moja na wanaume kupitia mada mbalimbali.

“Tunaungana nao na kuanzisha mada muhimu kupitia Mtandao wa Ushiriki wa Wanaume Tanzania (MenEngage Tanzania) chini ya uratibu wa shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) na leo tumefanya mdahalo wa kijamii kuhusu athari za ubaguzi wa kijinsia kwa takribani wanaume 50 wa eneo hili la kitunda,” anasema Mziray.

Anasema wamekuwa wakizungumza na wanaume katika mada mbalimbali kwa kuangalia mchango wao katika masuala ya kijamii, ikiwemo masuala ya malezi, wanaume ambao wamekuwa wakizungumzwa sana kukosekana kwenye malezi na masuala ya ukatili.

“Tulianzisha hivi vijiwe kuwafuata hukuhuku waliko, maana wengi wanasema wanakimbia nyumbani kwa kuwa kuna kelele, tuliwafuata huku kuona ni namna gani wanaume wana mchango katika jamii, hasa kubadilisha masuala ya malezi.

“Wanaume wengi wamekuwa hawashiriki kwenye malezi kwa familia, huku wengine wakiamini ni kazi za kinamama. Mijadala hii imeanza kuibua hoja mbalimbali na wanasema kwa nini hawashiriki katika malezi ya watoto majumbani,” anasema.

Mziray anasema wanachokitafuta katika vijiwe hivyo ni kuona namna gani wanaume wanashiriki kwenye masuala ya malezi, ndoa na kutatua migogoro ya familia.

Anasema wamekuwa wakiendesha midahalo hiyo kwa ushirikiano na mashirika mengine sita ambayo ni Makangarawe, Comprehensive Support to Persons with Disabilities (COSUPED), Hope 4 Young Girls Tanzania, Gender and Adolescent Initiative (GAI), na Youth of United Nations Association of Tanzania (YUNA).

Related Posts