Masauni awapa ujumbe wa haki Polisi, vigogo wizarani

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Hamad Masauni amewataka maofisa wa wizara hiyo likiwemo Jeshi la Polisi kuhakikisha wanabeba matatizo ya wananchi kama ya kwao.

Amewataka wafanye hivyo kwa kujua, wana dhima kubwa kwa Mungu na kwamba kuna maisha baada ya nafasi walizonazo.

Kauli hiyo ya Masauni inakuja katika kipindi ambacho, kumekuwa na malalamiko dhidi ya mwenendo wa utendaji wa Jeshi la Polisi ambapo baadhi wakilihusisha na vitendo viovu dhidi ya wananchi.

Masauni ametoa kauli hiyo usiku wa jana Jumamosi, Septemba 7, 2024, alipokuwa akizungumza kwenye semina elekezo kwa viongozi waandamizi wa wizara hiyo,  iliyofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema hatafumbia macho malalamiko ya dhuluma wanazofanyiwa wanyonge na masikini kwa sababu tu hawana fedha.

“Wananyanyasika kwa sababu hawana fedha. Lazima tujue tuna dhima kubwa sana, hii wizara tuliyonayo ina dhima kubwa sana kwa wale tunaoamini kuwa kuna Mungu kwamba kuna maisha mengine baada ya haya,” amesema.

Masauni amewataka maofisa wa wizara hiyo kuhakikisha wanabeba matatizo ya watu kama ya kwao

“Fikiria yeye ndiyo waziri halafu mimi ndiyo yeye, nimedhulumiwa nimenyanyaswa nakwenda sehemu ambayo natakiwa nipewe haki yangu sipewi, sisikilizwi sio sawa na wala sio falsafa ya 4R hiyo,” amesema.

Amesisitiza ni imani yake baada ya mafunzo hayo penye kasoro watakwenda kurekebisha na wasimamizi watachukua hatua dhidi ya maovu ya wale wa chini yao.

Amesema kwa jinsi mafunzo yalivyofanyika, wataibeba dhamana hasa katika kipindi cha kueleza uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

“Wizara hii ni tegemeo kubwa la kuhakikisha tunaingia katika uchaguzi, nchi yetu ikiendelea kubaki salama,” amesema.

Related Posts