Katika kuhakikisha nyota wake wanaozitumikia timu za taifa wanaziwahi mechi zao za ugenini za mashindano ya klabu Afrika wiki ijayo, Yanga na Simba zimepanga utaratibu wa wachezaji hao wanaungana na vikosi vyao moja kwa moja wakitokea katika majukumu ya timu zao za taifa na sio kuondoka nao pamoja kutokea hapa Dar es Salaam.
Kwa sasa Yanga imetoa wachezaji 14 wanazozitumikia timu saba tofauti za taifa huku Simba ikiwa na wachezaji wanne wanaozichezea timu mbili tofauti za taifa.
Wachezaji 14 wa Yanga waliopo katika timu za taifa ambazo kwa sasa zinacheza mechi za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 ni Clement Mzize, Abuutwalib Mshery, Mudathir Yahya, Dickson Job, Ibrahim Hamad, Nickson Kibabage na Bakari Mwamnyeto wanaoichezea Taifa Stars, Kennedy Musonda na Clatous Chama wanaoitumikia Zambia, Khalid Aucjo (Uganda), Stephane Aziz Ki (Burkina Faso), Djigui Diarra (Mali), Duke Abuya (Kenya) na Prince Dube (Zimbabwe).
Kwa Simba, wachezaji wao wanne ni Mohamed Hussein, Ally Salim na Edwin Balua ambao wanaitumikia Taifa Stars na Moussa Camara ambaye yupo na kikosi cha Guinea.
Mechi za mwisho za timu za taifa kucheza raundi ya pili ya hatua ya makundi ya kuwania kufuzu Afcon zitachezwa Jumanne Septemba 10 na baada ya hapo wachezaji watarejea katika klabu zao.
Siku tatu baada ya mechi hizo za raundi ya pili ya kuwania kufuzu Afcon, Simba itakuwa ugenini huko Libya katika mechi yake ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika na siku moja baadaye, Yanga itakuwa ugenini dhidi ya CBE ya Ethiopia katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ili kuwapuesha wachezaji wao na uchovu wa safari na kutumia muda mrefu angani, Simba na Yanga zimefiklia uamuzi wa kuungana na wachezaji hao katika nchi ambazo zitaenda kucheza kama ilivyothibitisha na mameneja wa timu hizo.
“Ratiba sio rafiki hivyo ni wachezaji wawili tu au watatu ambao ndio wataungana na timu Dar es Salaam wakitokea katika majukumu ya timu zao za taifa na kisha kuondoka pamoja lakini wengine wataungana na kikosi hukohuko Ethiopia,” alisema meneja wa Yanga, Walter Harrison.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema,”Kwa mazingira yaliyopo, hao wachezaji wataungana na timu kutokea hukohuko kwa vile tukisema warudi hapa wanaweza kupishana na timu ambayo inaweza kusafiri Jumanne au Jumatano.”
Wachezaji 10 wa Simba na Yanga waliopo na kikosi cha Taifa Stars, watamalizia majukumu yao ya timu ya taifa wakiwa huko Yamoussokrou, Ivory Coast ambako Septemba 10, watacheza dhidi ya Guinea ambayo yupo Moussa Camara.
Clatous Chama na Kennedy Musonda wao Septemba 10, timu yao ya taifa ya Zambia itakuwa nyumbani kuikabili Sierra Leone wakati Aucho atamalizia majukumu yake akiwa na kikosi cha Uganda, Jumatatu, Septemba 9 watakapokuwa nyumbani kuikabili Congo.
Duke Abuya na Djigui Diarra watamalizia majukumu yao ya timu za taifa Septemba 10 wakiwa Afrika Kusini ambako Kenya itacheza na Namibia na Mali itakabiliana na Eswatini huku Dube akimalizia majukumu yake akiwa Uganda ambako Zimbabwe itacheza na Cameroon.
Stephane Aziz Ki yeye, Septemba 10 timu yake ya Burkina Faso itakabiliana na Malawi huko Bamako, Mali